Kamishna Mkuu, baada ya kupokea pingamizi, kwa mujibu wa kifungu cha 12, ataamua pingamizi kama lilivyowasilishwa au anaweza kuitisha ushahidi wowote kadri atakavyoona inafaa kwa ajili ya kutolea uamuzi, na kwa msingi huo anaweza–

   (a) Kurekebisha makadirio kwa mujibu wa pingamizi;

   (b) Kurekebisha makadirio kwa mujibu wa ushahidi wowote uliopokelewa; au anaweza kukataa kurekebisha makadirio ya kodi.

Pale ambapo Kamishna Mkuu amekubali kurekebisha makadirio kwa misingi ya pingamizi atatoa waraka wa makadirio ya mwisho kwa mtoa pingamizi. Au-

   (a) Atapendekeza marekebisho kwa kuzingatia pingamizi na vielelezo vingine vilivyoletwa; au

   (b) Atapendekeza kukataa kurekebisha makadirio na atamtumia waraka mtoa pingamizi akieleza sababu za kukataa.

Baada ya kupokea waraka/taarifa mtoa pingamizi, ndani ya siku 30 atawasilisha waraka wa maandishi kwa Kamishna Mkuu kueleza kukubaliana au kupinga mapendekezo ya makadirio yaliyorekebishwa au yaliyokataliwa.

Kamishna Mkuu anaweza, baada ya kupokea waraka wa mtoa pingamizi kufanya yafuatayo:

(a) Kuamua kuhusu pingamizi kwa kuzingatia mapendekezo ya makadirio yaliyorekebishwa au yaliyokataliwa na wasilisho lolote lilifanywa mtoa pingamizi; au

(b) Kuamua kuhusu pingamizi kiasi fulani kwa kuzingatia wasilisho la mtoa pingamizi; au

(c) kuamua kuhusu pingamizi kwa mujibu wa marekebisho yaliyopendekezwa au yaliyokataliwa.

Pale ambapo mtoa pingamizi hajajibu mapendekezo ya Kamishna Mkuu ya kurekebisha makadirio au pendekezo la kukataa kurekebisha makadirio yaliyotolewa kulingana na kifungu kidogo cha (3), Kamishna Mkuu ataendelea kufanya makadirio ya mwisho ya kodi na kumpatia mtoa pingamizi taarifa kuhusu maamuzi yaliyotolewa.