Stempu za Kodi za Kilektroniki (ETS)

Matumizi ya stempu za Kodi za kielektroniki kwa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa yalitambulishwa ili kuondoa stempu za karatasi za kawaida ambazo zilihusishwa sana na ukwepaji wa Kodi na ugushaji wa stempu hizo.

Hii ni moja ya hatua za Serikali katika kuimarisha usimamizi wa kodi ndani ya nchi. Matumizi ya Stempu za Kodi za Kielektroniki itasaidia Serikali kutatua vikwazo vya muda mrefu katika kusimamia ushuru wa bidhaa. Mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki utasaidia Serikali, Wazalishaji/Waagizaji toka Nje na Walaji kama ifuatavyo:

(i)          Kulinda mapato ya Serikali   kwa kukomesha ugushaji wa stempu

(ii)         Kulinda maslahi ya walaji sababu mfumo unawezesha uhalali wa stempu kukaguliwa kwa kutumia simu ya mkononi.

(iii)        Kuwezesha ulipaji wa kodi kwa hiyari kwa wafanyabiashara wote ndani ya tasnia ili kutengeneza uwanja sawa wa ushindani wa kibiashara.

(iv)        Unawezesha ufatiliaji wa bidhaa kuanzia eneo la uzalishaji au forodha mpaka eneo la mwisho la mauzo.

(v)        Unasaidia kuhasibu uzalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru zulizozalishwa nchini au zilizoingizwa toka nje.

Bidhaa ambazo Stempu za Kodi za Kielektroniki Zinahusika.

Stamp za Kodi za Kielektroniki zinatumika katika baadhi ya bidhaa zilizochaguliwa zinazotozwa ushuru. Aina ya bidhaa hizi zitakuwa zikibadirika kadri ya muda ili kuimalisha usimamizi wa ushuru katika bidhaa hizo. Kwa sasa Stampu za Kodi za Kelektriniki zinatumika katika bidhaa zlizoingizwa toka nje au zilizozalishwa ndani ya nchi kama ifuatavyo:

(i)          Mvinyo na Pombe kali

(ii)         Maji ya Kunywa yaliyofungashwa katika chupa

(iii)        Sigara

(iv)        Sharubati (Juisi)

(v)         Bia

(vi)        Vinywaji laini

(vii)       Vinywaji Vikali

(viii)     Vilainishi

(ix)        Bidhaa za filamu na muziki (zilizorekodiwa).

(x)         Mafuta ya Mgando (Petroleum Jelly)

(xi)        Marashi (Perfumed Product)

 

 

Kumbuka:

Kwa sababu za kiutendaji, tarehe rasmi za kuanza matumizi stempu za kodi za kielektroniki zilipangwa kwa awamu. Awamu ya kwanza ya matumizi ilianza tarehe 15 Januari, 2019 ikihusisha bidhaa za sigara, mvinyo, pombe kali, bia na aina zote za vileo. Awamu ya pili ilianza rasmi mnamo tarehe 15 Agosti, 2019 ikihusisha bidhaa za juisi, maji na vinywaji vyote visivyo vya kileo.

 

Utoaji wa Leseni na Usajili wa Wazalishaji na Waagizaji

Wazalishaji wote na waagizaji wa bidhaa ambazo Stempu za Kodi za Kielektroniki zinahusika wanatakiwa kusajiliwa na Kamishna kabla ya kuzalisha au kuingiza toka nje bidhaa hizo. Wanatakiwa kufanya maombi ya kusajiliwa ambayo yatapitia uhakiki na Kamishna baada ya kuhakiki na kuridhika atatoa Hati ya Kusajiliwa. Hivyohivyo wazalishaji na waagizaji watapewa leseni na Mamlaka zinazowasimamia kwa kadri ya matakwa  ya Sheria zinazotumika.


 
Maombi na malipo ya idadi ya stempu za kodi za kielektroniki

Wazalishaji na waagizaji wa bidhaa zinazotakiwa kubandikwa stempu za kodi za kielektroniki wanatakiwa kutuma maombi ya stempu ndani ya siku 90 kabla ya kuzalisha au kuagiza bidhaa kutoka nje. Malipo ya tozo za stempu hizo yatafanyika baada ya Kamishna kuidhinisha maombi husika. Hata hivyo, Kamishna anaweza kuomba uthibitisho wa uingizaji bidhaa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kabla hajatoa stempu za kieletroniki.

Aidha, ili kurahisisha taratibu za kiutawala, mzalishaji au muagizaji wa bidhaa anatakiwa kutoa taarifa kwa Kamishna, angalau siku 90 kabla ya kuanza kwa kila mwaka wa fedha, juu ya makadirio ya idadi ya stempu za kodi za kielektroniki ambazo mzalishaji na/au muagizaji anatarajia kutumia katika katika mwaka wa fedha husika.

 

Mahali na muda wa kubandika stempu za kodi za kieletroniki

Stempu za kodi za kielektroniki kwa bidhaa zinazozalishwa nchini zitabandikwa stempu katika eneo la uzalishaji mara baada ya kufungashwa. Kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinatakiwa kubandikwa stempu ndani ya siku 14 baada ya kupata kibali kutoka mamlaka ya Forodha kwa ajili ya matumizi ya ndani. Kwa upande mwingine, stempu za kodi za kielektroniki zitabandikwa kwenye maeneo ambayo yatakuwa yametengwa na Kamishna. Hata hivyo, Kamishna anaweza kuruhusu bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kubandikwa stempu katika maeneo ya uzalishaji katika nchi husika kwa kufuata masharti yatakayotolewa na Kamishna.

 

Utoaji taarifa za matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki

Kila mzalishaji au muagizaji anatakiwa kutoa taarifa za matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki kwa kila mwezi.Kwa stempu zote zitakazokuwa zimeharibika zitatakiwa kutunzwa vizuri ili afisa anayehusika aweze kuzihakiki. Kwa mzalishaji au muagizaji ambaye hataweza kuzitolea taarifa za matumizi stempu za kodi za kielektroni ambazo atakuwa amepewa, Kamishna atakokotoa ushuru wa bidhaa kwa stempu hizo kwa kuzingatia kiwango cha juu cha kodi ya ushuru wa bidhaa na pia atakokotoa kodi nyingine zinazohusika kwa kuzingatia thamani au ujazo wa bidhaa zinazohusiana na stempu hizo. Katika kukokotoa ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa ambazo hazijaweza tolewa taarifa ya matumizi, Kamishna ataruhusu upotevu na uharibifu kwa kiwango kisichozidi 1% ya stempu hizo.

Urejeshaji wa stempu ambazo hazijatumika

Mzalishaji au muagizaji anatakiwa kurejesha stempu zote ambazo hazijatumika kwa Kamishna kutokana na sababu zifuatazo: -

i)            Mzalishaji ameacha kuzalisha bidhaa;

ii)           Muagizaji ameshindwa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi;

iii)          Dosari imegundulika katika stempu za kodi za kielektroniki; na

iv)          Kamishna akisitisha matumizi ya stempu za kieletroni zilizopo

Stempu za kodi za kielektroniki zikirejeshwa kutokana na kusitishwa matumizi yake na Kamishna, mzalishaji au muagizaji wa bidhaa atarudishiwa fedha ya tozo ya stempu hizo ndani ya siku 90.

Uhamisho wa stempu za kodi za kielektroniki

Mzalishaji anaweza kuhamisha stempu za kielektroniki kwenda eneo lake lingine la uzalishaji mara baada ya kupata kibali cha Kamishna. Mzalishaji au muagizaji akihamisha stempu bila kibali cha Kamishna atakuwa ametenda kosa kwa mujibu wa sheria. 

Uhakiki na uthibitisho wa stempu za kodi za kielektroniki

Mzalishaji, muagizaji, msambazaji na mfanyabiashara wa rejareja atakayehusika na kusambaza bidhaa zinazostahili kubandikwa stempu za kodi za kielektroniki, atatakiwa kuhakiki na kuthibitisha uhalali wa stempu za kielektroniki zilizopo kwenye bidhaa hizo kabla ya kuzipokea kataika hifadhi yake au kujihusisha nazo kwa namna yoyote ile.

Marufuku na makosa yanayohusiana na stempu za kodi za kielektroniki

Adhabu ya makosa yanayohusiana na stempu za kodi za kielektroniki ni pamoja na kifungo, faini au vyote kwa pamoja. Makosa hayo ni pamoja na yafuatayo: -

   i).        Uingizaji wa bidhaa zinazostahili kubandikwa stempu za kielektoniki pasipo kusajiliwa na Kamishna;

  ii).        Kushindwa kutunza kumbukumbu na rejesta za stempu za kielektroniki kama ilivyoelekezwa na Kamishna;

 iii).        Kushindwa kubandika stempu za kodi za kielektroniki katika vifungashio vya bidhaa katika hali ya usalama kama ilivyoelekezwa na Kamishna;

 iv).        Kuchapisha juu ya stempu au kubadili muonekano wa stempu iliyobandikwa kwenye kifungashio cha bidhaa;

  v).        Kuwasilisha ritani isiyo sahihi kwa makusudi;

 vi).        Kushindwa kutoa taarifa yoyote ambayo itahitajika na Kamishna;

vii).        Kumiliki bidhaa zinazostahili kubandikwa stempu za kielektroniki pasipo kubadikwa stempu hizo;       

viii).        Kujaribu kujipatia au kujipatia stempu za kilektroniki kwa njia isiyo halali bila kuwa na kibali cha Kamishna;

 ix).        Kughushi; kuchapisha au kutengeneza stempu za kilektroniki bila kibali cha Kamishna;

  x).        Kumiliki stempu za kilektroniki bila kuwa na kibali cha Kamishna; na

 xi).        Kumiliki, kusafirisha, kusambaza na kuuza bidhaa zinazostahili kubandikwa stempu pasipo kubandikwa stempu za kielektroniki.

Mtu yeyote atayekutwa na hatia ya kosa au makosa yaliyotajwa ataadhibiwa kwa kifungo kisichozidi miaka mitatu (3), au faini isiyopungua shilingi milioni 5 na isiyozidi shilingi milioni 50 au vyote kwa pamoja.