Utangulizi:

Kodi ya zuio ni kiasi cha kodi kinachozuiwa na mtu anapomlipa mtu mwingine kutokana na bidhaa zilizosambazwa au huduma iliyotolewa na mlipwaji. Mtu anayepokea au anayestahili kupokea malipo ambayo kwayo kodi ya mapato inatakiwa kuzuiwa ni mkatwaji wa kodi ilhali mtu anayepaswa kuzuia kodi ya mapato kutoka katika malipo yaliyofanyika kwa mkatwaji anajulikana kama Wakala wa kodi ya zuio.

 

Malipo yanayostahili kukatwa kodi ya zuio

Kodi ya zuio inatozwa katika malipo husika ikiwa ni pamoja na malipo yanayopaswa kujumuishwa katika kukokotoa mapato ya mwajiriwa yanayostahili kukatwa kutoka kwa mwajiriwa katika ajira, malipo ya mapato ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na magawio, riba, malipo ya maliasili, pango au mrabaha, malipo ya huduma na malipo ya mikataba na malipo ya bidhaa zilizosambazwa serikalini na kwenye taasisi zake.

 

Taarifa na Muda wa Kulipa Kodi Iliyozuiwa

  • Kila wakala wa kodi ya zuio atalipa kwa Kamishna kodi ya zuio aliyozuia ndani ya siku 7 baada ya kila mwisho wa mwezi wa kalenda.
  • Kila wakala wa kodi ya zuio atapeleka kwa Kamishna ndani ya siku 30 baada ya kipindi cha kila miezi sita ya kalenda taarifa katika fomu maalum iliyoandaliwa inayobainisha malipo yaliyofanywa na wakala katika kipindi husika cha zuio la kodi, jina na anwani ya mzuiwa, kodi ya mapato iliyozuiwa kutoka katika kila malipo yaliyozuiwa; na taarifa nyingine yoyote ambayo Kamishna ataelekeza.

 

 

Hati ya Kodi ya Zuio

Wakala wa kodi ya zuio ataandaa na kumtunuku mzuiwa hati ya kodi ya zuio ikionesha kiasi cha malipo alicholipwa mzuiwa na kodi ya mapato iliyozuiwa kutoka katika malipo hayo. Hati ya zuio itahusisha mwezi wa kalenda na itatolewa ndani ya siku 30 baada ya mwisho wa mwezi. Hata hivyo, kwa upande wa kodi inayozuiwa kutoka katika kodi ya ajira hati itahusisha sehemu ya mwaka wa kalenda katika kipindi ambacho mwajiriwa atakuwa amejiriwa na atahudumiwa ifikapo tarehe 30 ya Januari baada ya mwisho wa mwaka au, pale ambapo ajira yake imesitishwa na wakala wa zuio katika mwaka si zaidi ya siku 30 kutoka tarehe ambayo ajira ilisitishwa.

 

Aina za Kodi za Zuio

Sheria imegawanya kodi ya zuio katika aina kuu mbili, ambazo ni:-

  • Kodi za Zuio za mwisho
  • Kodi za Zuio zisizo za Mwisho

Kodi za Zuio za Mwisho ni kodi ambazo mzuiwa hawezi kudai punguzo lolote la kodi wakati wa kukokotoa kodi ya mapato inayolipwa kwa mwaka wa mapato.

Kodi za Zuio zisizo za Mwisho: ni kodi ambazo mzuiwa anastahili punguzo la kodi kiasi sawa na kodi inayochukuliwa kuwa imelipwa kwa mwaka wa mapato ambamo kiasi hicho kimekokotolewa.

 

VIWANGO VYA KODI YA ZUIO 

Chanzo cha kodi

Mkazi

Asiye mkazi

Magawio kwa makampuni yanayomiliki hisa kwa 25% au zaidi

5%

Hakuna

Magawio kutoka kwenye makampuni yaliyoorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam

5%

5%

Magawio kutoka kwenye makampuni mengine

10%

10%

Malipo mengine ya kodi ya zuio

15%

15%

Riba

10%

10%

Mirabaha

15%

15%

Huduma za kiutawala na kiufundi (Uchimbaji Madini, Mafuta na Gesi)

  5%

15%

Watoa huduma za usafirishaji (Ndege/Meli) wasio wakazi/wakodisha ndege wasio na makazi ya kudumu

Hakuna

5%

Mapato kutokana na ukodishaji wa nyumba/majengo

10%

15%

Malipo ya bima

0%

5%

Malipo yatokanayo na maliasili

15%

15%

Ada za huduma

5%

15%

Faida ya kuuza hisa, ardhi na majengo

10%

20%

Malipo ya Wakurugenzi (wakurugenzi wasio na ajira za kudumu) 

15%

15%

Asilimia ya faida inayotolewa kwa wakala kutoka kwa watoa huduma za utumaji fedha kwa njia ya simu za mkononi. 10% Hakuna
Malipo kwa bidhaa zilizosambazwa na mtu yeyote kwa serikali na taasisi zake. 2% kabla ya kukatwa Kodi Haihusiki
Kodi ya Pango 10% 15%

  

Fomu

ITX234.01.E Hati ya Kodi ya Zuio kwenye ada za huduma

Hati/stakabadhi ya malipo kwa ajili ya kodi ya zuio kwa ada za huduma

ITX 230.01.E Taarifa ya kodi ya zuio

Taarifa ya kodi ya zuio na malipo ya kodi iliyozuiwa

ITX 302.01.E Hati/ stakabadhi ya malipo; Kodi ya Zuio kutoka katika riba ya benki.

Hati/ stakabadhi ya malipo kwa ajili ya kodi ya zuio iliyokatwa kutoka kwenye riba ya benki.