Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi

 Utangulizi:

Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi: ni kodi inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania chini ya Sheria ya Mafunzo ya Ufundi Stadi na Sheria ya Kodi ya Mapato.

Utozaji: Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi inatozwa kwa kuzingatia malipo-ghafi ya malipo yote  yanayofanywa na mwajiri kwa waajiriwa walioajiriwa  na mwajiri huyo katika kipindi mahususi. Ni muhimu kuelewa kuwa Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi ni wajibu na hulipwa na mwajiri.

Malipo –ghafi ni jumla ya mishahara, ujira, malipo ya likizo, ada, kamisheni, bonasi, kiinua mgongo, posho yoyote ya safari, viburudisho, au posho nyingine anazopokea mwajiriwa kutokana na ajira yake au huduma aliyotoa. 

Pale inapotokea mwajiri anamlipa malipo mwajiriwa yeyote kwa muda wa chini ya mwezi mmoja au kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja, malipo hayo yatachukuliwa kana kwamba mwajiriwa huyo alikuwa anastahili malipo ya kila mwezi na kiasi cha malipo yanayotozwa kodi kwa mwezi kwa mwajiriwa huyo kwa mwezi wowote kitachukuliwa kuwa ni malipo yanayotozwa kodi iwapo mwajiriwa huyo angelipwa mshahara wa kila mwezi.

Ni Nani Anawajibika Kulipa Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi?

Mwajiri yeyote anayeajiri wafanyakazi kumi au zaidi atalipa kodi ya kuendeleza Ufundi Stadi kulingana na mishahara ghafi.

 Viwango Stahiki:

Kiwango kinachotakiwa kwa kodi ya kuendeleza Ufundi Stadi ni 4% ya jumla ya ujira waliolipwa waajiriwa wote katika kipindi cha mwezi.

Waajiriwa wanajumuisha waajiriwa wa kudumu, wa muda, waajiriwa wa ziada, vibarua  n.k.

 Wajibu wa Mwajiri:

·         Kukokotoa kiwango cha kodi na kukilipa katika akaunti ya Kamishna katika mkoa husika wa kodi ambamo mwajiriwa amesajiliwa.

·         Malipo ya tozo ya Kuendeleza Ufundi Stadi yatafanyika kwa kutumia fomu ITX 300.01.E – Karatasi ya Malipo ya Kodi za Ajira.

·         Kuandaa taarifa ya mapato ya mwezi na kuwasilisha katika ofisi ya Mamlaka ya Mapato ifikapo au kabla ya siku ya 7 ya mwezi unaofuata.

·         Kuandaa na kutuma hati ya nusu mwaka inayolingana na taarifa ya mapato ya kila mwezi iliyowasilishwa katika kipindi hicho.

Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi haitatozwa kwa: -

(a)    Idara ya serikali au taasisi ya umma ambayo inaendeshwa kwa ruzuku ya serikali;

b)     Ofisi za Kidiplomasia;

(c)    Umoja wa Mataifa na Mashirika yake;

(d)    Taasisi za kimataifa na taasisi nyingine za kigeni zinazojishughulisha na utoaji misaada au misaada ya kitaalamu;

(e)   Asasi za kidini ambazo waajiri wake wameajiriwa tu katika:

        (i) kusimamia maeneo ya ibada

        (ii) kutoa maelekezo ya kidini au kusimamia masuala ya kidini

        (iii) kutoa huduma za afya

(f) Mashirika ya misaada

(g) Mamlaka za serikali za mitaa.

(h) Waajiri wenye mashamba ambao  waajiriwa wao wanajishughulisha  moja kwa moja katika kilimo na hawatajumuisha waajiriwa ambao wanahusika na usimamizi wa shamba au usindikaji wa mazao ya shambani. 

(i) Taasisi na Vyuo vya Elimu vilivyosajiliwa (Shule binafsi zikiwemo shule za awali, za Msingi, Sekondari, Shule za Mafunzo ya ufundi standi, Vyuo vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu.)

Shirika la misaada ni asasi ya umma ya ndani ya nchi iliyosajiliwa kwa ajili hiyo na inajishughulisha kiupekee kwa ajili ya:

     (a) kupunguza umaskini au matatizo ya umma;

     (b) utoaji wa elimu au afya ya umma; na Kamishna Mkuu baada ya kufanya uchunguzi wa kutosha amejiridhisha kuwa shughuli inayofanywa na asasi hiyo ni kwa manufaa ya umma

 Zingatia

i) Jumla ya malipo ni majumuisho ya mshahara,malipo ya likizo,kamisheni,mafao,bonasi,malipo ya kujikimu,usafiri,malipo ya kujiburudisha au malipo yoyote yanayoendana na utendaji kazi husika isipokuwa malipo yale yaliyotumika katika utekelezaji wa moja kwa moja wa kazi ya mwajiri.

ii) Msamaha kwa Zanzibar itahusishwa Taasisi/Idara zilizopo kipengele s)-d) na g)