1.        Utangulizi:

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inapenda kuwahakikishia Wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kuwa utaratibu wa kutumia Mashine za EFD ulianzishwa kwa lengo la kumrahisishia mfanyabiashara utunzaji wa kumbukumbu za biashara za kila siku pamoja na kuondoa usumbufu wakati wa ukadiriaji wa kodi.

2.        Walengwa

Mfumo huu wa kutumia mashine za kodi za kielektroniki ulianza kutekelezwa kwa awamu. Awamu ya kwanza ilianza mwaka 2010 kwa wafanyabiashara waliosajiliwa kwenye kodi ya ungezeko la thamani, yaani VAT.

Awamu ya pili imeanza kutekelezwa mwaka huu 2013 ikiwahusu wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa kwenye VAT ambao Mauzo ghafi kwa mwaka ni shilingi milioni 14 na zaidi. Sheria ya kusimamia awamu hii ya pili ni ya Kanuni ya Kodi ya Mapato (Income Tax Electronic Fiscal Devices Regulations, 2012).

Wafanyabiashara zisizo rasmi aina ya Mama Ntilie na wale wanaotembeza bidhaa barabarani hawahusiki kwa sababu hawana sehemu maalum ya kufanyia biashara. Hawa waendelee na shughuli zao na wala hawatabughudhiwa. Wanaolengwa ni wenye biashara wenye mauzo ya milioni 14 na zaidi, kwa mfano wenye biashara zifuatazo;

a)    Wenye  maduka ya vipuri

b)    Mawakili

c)    Maduka ya jumla (Sub wholesale shops)

d)    Wafanyabiashara wakubwa wa Mbao

e)    Migahawa mikubwa

f)    Maduka ya simu na vipuri vyake

g)    Baa na vinywaji baridi

h)    Studio za picha

i)     “ Catering Services”

j)     Wauzaji wa Pikipiki

k)    Maduka makubwa ya nguo.

l)     Na biashara zinginezo

Kwa Nchi nzima tumelenga wafanyabiashara laki mbili tu kwa awamu ya pili  kati ya wafanyabiashara zaidi ya milioni moja na nusu ambao wamesajiliwa kulipa kodi.

 3.        Faida  za Mashine za Kodi za Kielekitroniki

 • Kutoa risiti na Ankara za kodi. Kwa kuwa sheria inamtaka kila mfanyabiashara anayeuza au kutoa huduma atoe risiti, mfanyabiashara huyu alilazimika kuchapisha vitabu vya risiti mara zote, kwa kutumia mashine hizi anaondokana na uchapishaji wa vitabu ambavyo ni vingi na utunzaji wa nakala zake unaleta usumbufu.
 • Hutumia lugha ya Kingereza na Kiswahili hivyo kumrahisishia mtumiaji kuchagua lugha anayoitaka.
 • Zina uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu za mauzo, manunuzi na mali ya biashara (Stock) bila kufutika kwa muda usiopungua miaka mitano na hivyo kuondokana na usumbufu wa kuchapisha vitabu vya risiti kwa kipindi chote hicho.
 • Kumuwezesha mtumiaji kutoa taarifa za mauzo kwa siku, wiki, mwezi na mwaka, kwa kipindi kisichopungua miaka mitano.
 • Kutuma taarifa za mauzo moja kwa moja kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato au Mamlaka nyingine zenye mahitaji ya taarifa hizo kwa  mfano EWURA, SUMATRA, Benki Kuu au Idara ya Takwimu  kwa kuwa zimeunganishwa na mtandao ( GPRS)
 • Huweza kupokea maelekezo moja kwa moja kutoka kwenye mfumo wa Mamlaka ya Mapato “TRA Server” kuruhusu kuongeza uwezo wa hizi mashine Wakati wowote bila kuathiri matumizi/ ufanyaji kazi wake.
 • Huweza kutuma na kupokea ujumbe (SMS) kutoka kwenye mfumo wa Mamlaka ya Mapato. Hii huwezesha TRA kumtaarifu mtumiaji taarifa yoyote ya kodi inayomuhusu bila kuonana ana kwa ana.
 • Inaweza kutumika kutuma na kupokea fedha “mobile money” na kwa hiyo kumruhusu mtumiaji kuitumia kuongeza kipato zaidi au kulipa kodi na huduma zingine kama vile umeme, maji n.k bila kupoteza muda kwenda kwenye ofisi husika.

4.        Tuhuma kuhusu bei za mashine na matengenezo

Tuhuma kwamba mfumo wa EFDs ni mradi wa mtu au ni wa wafanyabiashara wachache sio za kweli kwani mchakato wa ununuzi wa  Mashine za EFD ulifanyika kwa uwazi kupitia tenda ya kimataifa na kila mtu alikuwa na uhuru kushiriki. Kati ya walioomba walipatikana wasambazaji 11 na sio mmoja au wachache kama inavyopotoshwa. Mchakato wa kuwapata wazabuni ulifuata Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004 inayotumika, na uligawanyika katika sehemu mbili kama ifuatavyo;

a)   Kuwapata watengenezaji wa Mashine; Tenda ya wazi ya Kimataifa (International bidding) ilitangazwa kupitia magazeti ya Daily News ya tarehe 10 Agosti 2012 na The East African ya tarehe 11-17 Agosti 2012.  Watengenezaji waliokidhi vigezo vilivyoainishwa ndio waliopata tenda. 

b)   Kuwapata wasambazaji; Tenda ya wazi ilitangazwa kwenye gazeti la Daily News la tarehe 10 Agosti 2012 kwa wasambazaji wenye vigezo vinavyojumuisha; wajibu wa kufungua ofisi kila mkoa, mtaji usiopungua Shilingi za Kitanzania milioni 500, uzoefu wa kusambaza na kufanyia matengenezo mashine za kielektroniki kwa zaidi ya miaka miwili. Wasambazaji waliokidhi vigezo vilivyoainishwa ndio waliopata tenda. 

 • Kwa kuzingatia umuhimu wa kutunza kumbukumbu kwa wafanyabiashara nchini, TRA pamoja na watengenezaji na wasambazaji wa mashine za kielektroniki walijadiliana na kuafikiana kwamba bei za mashine ziuzwe kuanzia TSHS 600,000/= na ukomo uwe TSHS 690, 000 kwa machine za ETR na kuanzia TSHS 1,000,000 na ukomo uwe TSHS 1,200,000 kwa mashine za EFP na ESD. Bei za mashine hizi hapa nchini zipo chini ukilinganisha na bei ya mashine katika nchi zinazotumia mfumo unaofanana na wa Tanzania.
 • Bei za EFD katika nchi nyingine duniani:

NCHI

Bei ya chini kwa dola za kimarekani

Bei ya juu kwa dola za kimarekani

Italy

870

1,000

Rwanda

800

830

Ethiopia

446

1,026

Serbia

360

1,750

Bulgaria

230

400

Tanzania

375

487

 

Ili kumrahisishia mfanyabiashara ununuzi wa mashine hizi, TRA imeongea na wasambazaji ambao wamekubali kuuza mashine hizi kwa kupokea malipo kwa awamu iwapo wafanyabiashara watajiunga katika vikundi vitakavyopewa dhamana ya kuhakikisha wauzaji wanapata malipo yao.

 

Kuhusu gharama za matengenezo kuwa kubwa, watengenezaji wametoa “warranty” ya miaka mitatu kwa mashine inayoharibika pasipo makusudi. Hivyo pale mashine inapoharibika mfanyabiashara anatakiwa kuwasiliana na mtengenezaji kwa ajili ya matengenezo. Wasambazaji wanawajibika kufunga mashine, na kutoa elimu bora ya matumizi ya mashine hizo.  Tungependa wafanyabiashara waelewe kuwa sheria inamtaka kila msambazaji pamoja na kuuza mashine anawajibika kuzifanyia matengenezo mashine hizo. Hii itasaidia kudhibiti taarifa ambazo zimo ndani ya mashine.

Ikumbukwe kuwa gharama zote za ununuzi wa mashine hizi zinarudishwa kwa wafanyabiashara pale watakapowasilisha mahesabu yao ya kodi. Hivyo kuifanya Serikali kulipia gharama za mashine kwa kupitia kodi ambayo itasamehewa pindi mfanyabiashara atakapowasilisha mahesabu.

 5.        Malalamiko kuhusu kutozwa kodi ya asilimia 18

Kumekuwepo na malalamiko kuwa utumiaji wa mashine hizi utasababisha wafanyabiashara kutozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18. Ukweli ni kwamba awamu ya kwanza ya uuzaji wa mashine hizi ndio ulilenga kwa wafanyabiashara walio sajiliwa kwenye kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na awamu hii haijalenga hao bali ni kwa ajili ya kodi ya mapato. Hivyo basi malalamiko hayo sio ya kweli na hakuna ongezeko lolote la kodi litakalosababishwa na utumiaji wa mashine hizi.  

 6.        Elimu

Kabla ya kuanza utekelezaji wa mfumo huu elimu ilitolewa kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na semina ambazo zilitolewa kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara. Elimu bado inaendelea kutolewa kwa njia mbalimbali ambapo kuhusu ununuzi wa mashine hizo kwa awamu ya pili muda wa maandalizi umesogezwa hadi kufikia tarehe 31 Disemba 2013 na taarifa imetolewa na inaendelea kutolewa katika vyombo vya habari.

 7.        Matapeli

Mamlaka ya Mapato Tanzania inapenda Kuufahamisha Umma kwamba kumejitokeza watu wanaojifanya ni watumishi wa TRA amabo hupita madukani na kuwasumbua wafanyabiashara kuhusiana na masuala ya matumizi ya mashine. Endapo watakutana na watumishi wa aina hiyo dai kitambulisho na nyuma ya kitambulisho kuna simu ya Mwajiri (TRA) tumia namba za simu ili kupata uthibitisho kama ni watumishi halali.

 8.           Wito

Mwananchi anaponunua bidhaa au huduma anatakiwa kudai risiti. Kwa kufanya hivyo, Kama asipopewa risiti kodi hiyo inaingia mfukoni mwa mfanyabiashara maana haitowasilishwa TRA na hivyo kuikosesha serikali mapato ambayo yangesaidia miradi ya maendeleo ya taifa na kuboresha huduma za jamii kwa wananchi.

Hata hivyo, Mamlaka ina habari kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wachache ambao hawataki kulipa kodi hivyo kuwashawishi na kuwachochea wafanyabiashara wengine kugoma kutumia mashine. Mamlaka inawataka kuacha tabia hiyo mara moja.

 9.            Mawasiliano

Simu bila malipo katika kituo cha Huduma

 • 0800 750075
 • 0800 780078