Ushuru wa bidhaa
Ushuru wa bidhaa ni kodi inayotozwa kwa bidhaa au huduma maalum zilizozalishwa ndani ya nchi au kuingizwa nchini kwa viwango tofauti. Kodi hii inatozwa katika viwango maalum na viwango kulingana na thamani.
Vitu vinavyotozwa viwango maalum ni pamoja na:
Mvinyo, vinywaji vikali, bia, vinywaji laini, maji ya chupa, juisi ya matunda, Dividii, Visidii, Sidii na kanda zilizorekodiwa sauti, sigara, tumbaku, bidhaa za petroli na gesi asilia.
Vitu vinavyotozwa kulingana na thamani yake ni pamoja na:
Huduma za kutuma na kupokea fedha, huduma za mawasiliano ya kielektroniki, malipo ya huduma za televisheni, samani zilizoingizwa kutoka nje, vyombo vya moto, mifuko ya plastiki, ndege maalum, silaha za moto, makasha maalum, vipodozi na dawa.
Viwango kulingana na thamani ni: 0%, 5%, 10%, 17%, 15%, 20%, 25% ,30% na 50%.
Wajibu wa kulipa ushuru.
Ushuru utakuwa ni lazima na utalipwa kwa kuzingatia:
(a) bidhaa yoyote iliyoingizwa na mwingizaji, wakati bidhaa hiyo haijakoma kuwa chini ya udhibiti wa forodha au wakati mwingine wowote kama itakavyokuwa imeelekezwa na Waziri mwenye dhamana katika Gazeti la Serikali,
(b) bidhaa yoyote iliyozalishwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na mzalishaji:
(i) baada ya kuuzwa kwa bidhaa na mhusika, au
(ii) baada ya bidhaa kukoma kuwa chini ya udhibiti wa forodha, au
(iii) baada ya kuondolewa kwa bidhaa katika eneo la uzalishaji, lolote litakalotokea kwanza.
(c) bidhaa yoyote iliyozalishwa au kuingizwa nchini na mtu yeyote bila kulipia ushuru na ambayo baadaye imeuzwa kwa mtu yeyote na mnunuzi wakati akiuza bidhaa hiyo;
(d) huduma yoyote ya mawasiliano ya kielektroniki iliyotolewa na mtoa huduma za mawasiliano wakati simu hiyo ya kiganjani, ya mezani au isiyotumia waya inatumika au wakati malipo yanapopokelewa kwa ajili ya huduma wakati wowote.
(e) malipo yoyote ya kumlipa mtoa huduma ya televisheni kwa njia ya setilaiti wakati huduma inapotolewa.