Taratibu za Kuweka Pingamizi na Kukata Rufaa

Mtu yeyote ambaye hakubaliani na makadirio ya kodi aliyofanyiwa anapewa nafasi kuwasilisha pingamizi la makadirio hayo. Pingamizi linapaswa kuwa katika maandishi na kutumwa kwa Kamishna Mkuu. Pia yawe na ujumbe ambao ni mahususi, ukielezea msingi wa pingamizi kwa makadirio yaliyofanywa.

Rufaa itakatiwa wapi na kuwasilishwa kwa nani?

Kamishna Mkuu katika mazingira ya kawaida kuhusiana rufaa ina maana:

Kamishna wa Forodha, Idara ya Walipa Kodi Wakubwa, na Kodi za Ndani. Hata hivyo ushughulikiaji wa rufaa unafanywa na mameneja wa maeneo husika.

 

Ushughulikiaji wa Kodi zenye Mgogoro

Itabidi kuwasilisha pingamizi kwa Kamishna Mkuu ndani ya siku 30 tangu siku ya kupokea makadirio kusubiri uamuzi wa mwisho. Wakati wa kipindi cha pingamizi kutegemea uamuzi wa mwisho wa pingamizi kwenye makadirio yaliyofanywa na Kamishna Mkuu, mlipakodi huyo anawajibika kisheria kulipa kiasi cha kodi ambacho hakipo kwenye mgogoro au theluthi moja ya kodi iliyokadiriwa, kiasi chochote kilicho kikubwa. Hata hivyo, ikiwa Kamishna Mkuu ataridhika kwamba kuna sababu za msingi kuruhusu kupunguza au kuondoa kodi itakayolipwa wakati wa pingamizi hilo anaweza kuagiza kuwa kiasi kidogo kilipwe  au asamehe kiasi kinachotakiwa cha malipo ya kodi.

Kodi ambayo haina mgogoro italipwa wakati wa kufungua shauri la pingamizi na kama tarehe ya kulipa imefika mapema kuliko kipindi cha siku 30 kodi ambayo haina mgogoro italipwa katika tarehe hiyo husika. Kiasi cha kodi kama kitakavyoamuliwa mwishoni baada ya kusuluhisha pingamizi hilo, kama kitakuwa kidogo kuliko kiasi kilicholipwa kwa Kamishna Mkuu kitarejeshwa kwa anayepinga. Kuhusu suala la kodi au ushuru uliokadiriwa kwenye kodi, kiasi chote kilichokadiriwa kitachukuliwa kuwa hakipo katika mgogoro.

Kuchelewa Kuwasilisha Pingamizi la Makadirio ya Kodi

Mlipakodi anaweza kushindwa kuweka pingamizi kwa wakati dhidi ya makadirio ya kodi. Hata hivyo, sheria bado inampa nafasi mtu huyu kuweka pingamizi baada ya kipindi husika kupita. Kamishna anaweza kukubali au kukataa pingamizi kutegemea kuridhishwa au kutoridhishwa  na sababu  za kuchelewa huko.