Kodi ya Ongezeko la Thamani ni nini?
Kodi ya Ongezeko la Thamani ni kodi ya mlaji inayotozwa katika bidhaa zinazostahili kutozwa kodi, ikiwa ni pamoja na huduma, mali zisizohamishika na shughuli yoyote ya kiuchumi wakati wowote thamani inapoongezeka katika kila hatua ya uzalishaji na katika hatua ya mwisho ya mauzo. Kodi ya Ongezeko la Thamani inatozwa kwa bidhaa zote zinazozalishwa ndani na huduma na kwenye maduhuli. Kodi ya Ongezeko la Thamani anatozwa mtu aliyesajiliwa kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani tu.
Mawanda ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ni yapi?
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) itatozwa kwenye usambazaji wowote wa bidhaa, huduma, na mali zisizohamishika zinazotokana na shughuli za kiuchumi Tanzania Bara ambapo kuna usambazaji unaotozwa kodi na mtu anayetozwa kodi katika muktadha wa shughuli hiyo. Hii inajumuisha uingizaji wa bidhaa zinazotozwa VAT zinazohusiana na mali zisizohamishika kwenye ardhi iliyoko Tanzania Bara. Uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya Tanzania Bara pia utatozwa VAT kwa mujibu wa sheria na taratibu za kawaida za Forodha. Usambazaji wa bidhaa au huduma zinazotumiwa nje ya Tanzania Bara utatozwa kiwango cha sifuri 0% endapo ushahidi utatolewa. Kiwango cha kawaida cha VAT ni 18%, wakati mauzo ya nje ya bidhaa na huduma yanatozwa VAT kwa kiwango cha 0%.
Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni wa lazima kwa mtu yeyote ambaye mauzo yake yanayotozwa VAT yanafikia TZS milioni 200 ndani ya kipindi cha miezi kumi na miwili (12), au TZS milioni 100 (nusu ya kiwango cha usajili) ndani ya kipindi cha miezi sita (6) kinachoishia mwishoni mwa mwezi uliotangulia.
Kiwango hiki cha mauzo hakihusu watoa huduma za kitaaluma, taasisi au idara za Serikali zinazofanya shughuli za kiuchumi, wala wafanyabiashara wanaotarajia kuanza biashara (intending traders) ambao wanawasilisha ushahidi wa kutosha wa nia yao ya kuanzisha biashara, kama vile mikataba, zabuni walizoshinda, michoro ya majengo, mpango wa biashara au uthibitisho wa ufadhili kutoka benki.
Mtu anayestahili kusajiliwa kwa VAT anatakiwa kuwasilisha maombi kwa Kamishna Mkuu ndani ya siku 30 tangu awe na wajibu wa kusajiliwa. Hata hivyo, mfanyabiashara anayetarajia kuanza biashara anaweza kuwasilisha maombi wakati wowote kabla ya kuanza shughuli za biashara.
Iwapo mtu anayestahili kusajiliwa kwa VAT atashindwa kuwasilisha maombi, Kamishna Mkuu anaweza kumsajili kwa hiari yake, bila kujali kiwango cha mauzo, endapo ataridhika kuwa usajili huo unahitajika, ikiwemo kwa madhumuni ya kulinda mapato ya Serikali. Mtu huyo ataarifiwa kuhusu usajili wake ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kusajiliwa.
Mchakato wa Usajili
Maombi ya usajili wa VAT yanafanywa kupitia Taxpayer Portal (Huduma za Mtandaoni za TRA) kwenye tovuti ya TRA baada ya mwombaji kuingia kwenye mfumo.
Cheti cha Usajili wa VAT
Baada ya kusajiliwa, mlipakodi atapewa Cheti cha Usajili chenye jina na makao makuu ya biashara ya mlipakodi, tarehe ya kuanza kwa usajili, Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na namba ya usajili ya VAT.
Mtu yeyote anatakiwa kuonyesha TIN na namba ya VAT katika fomu zote rasmi zinazohusiana na VAT, na kutundika cheti cha usajili mahali pa kuonekana katika makao makuu ya biashara yake.
Ritani ya VAT na Malipo ya Kodi
Ritani ya VAT ni tamko rasmi linalowasilishwa na mtu aliyesajiliwa kwa VAT kwa mamlaka ya kodi, likionesha taarifa za miamala yake ya VAT kwa kipindi maalum cha kodi, ambacho kwa kawaida huwa ni mwezi.
VAT inalipwa na mlipakodi aliyesajiliwa ifikapo au kabla ya tarehe 20 ya mwezi unaofuata, ambayo pia ndiyo tarehe ya mwisho ya kuwasilisha ritani ya VAT. Wakala wa ukataji wa zuio ya VAT anatakiwa kuwasilisha marejesho na kulipa VAT aliyozuia kwa Kamishna Mkuu ndani ya siku 10 baada ya kumalizika kwa kila kipindi cha kodi.
Viwango vya Kodi
Viwango vipi hutumika kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani?
Kodi ya Ongezeko la Thamani hutozwa katika bidhaa na huduma stahiki kwa viwango vifuatavyo :-
| Na. | Maelezo ya Huduma/Bidhaa | Kiwango cha VAT |
|---|---|---|
| 1. | Usambazaji wa bidhaa na huduma Tanzania Bara | 18% |
| 2. | Uingizaji wa bidhaa na huduma Tanzania Bara | 18% |
| 3. | Gharama za ugavi kupitia benki au mfumo wa malipo wa kielektroniki ulioidhinishwa na Kamishna Mkuu kwa mtu ambaye hajasailiwa na Kodi ya Ongezeko la Thamani | 16% |
| 4. | Mauzo ya nje ya bidhaa/huduma | 0% |
| 5. | Kutomhusisha mpitishaji bidhaa kulipa VAT kwa gharama ya huduma ya usafirishaji wa bidhaa/mizigo iendayo nje ya nchi kupitia Tanzania Bara, huduma zinajumuisha:- | |
I. Huduma zinazohusiana moja kwa moja na bidhaa inayopitishwa kwenda nje ya nchi
| 0% | |
| II. Bidhaa zilizohifadhiwa kwenye bandari, uwanja wa ndege au maeneo ya forodha kwa kipindi kisichozidi siku 30 zikisubiri kusafirishwa | 0% | |
| 6. | Bidhaa kwa wakala wa kukata VAT | 15% |
| 7. | Huduma kwa wakala wa kukata VAT | 12% |
Kodi ya Ongezeko la Thamani inatozwaje?
Mfumo wa VAT unafanya kazi kwa njia ya kukata kodi iliyolipwa dhidi ya kodi iliyokusanywa. Kila mfanyabiashara aliyesajiliwa VAT hulipa VAT anaponunua bidhaa au huduma (VAT ya manunuzi) na hutoza VAT anapouza bidhaa au huduma (VAT ya mauzo). Mfanyabiashara hulipa TRA tofauti iliyobaki kati ya VAT aliyokusanya kwenye mauzo na VAT aliyolipa kwenye manunuzi. Ikiwa VAT ya manunuzi ni kubwa kuliko VAT ya mauzo, mfanyabiashara anaweza kudai salio hilo kama punguzo au kurejeshewa kutoka TRA. Kwa ujumla, VAT si gharama kwa wafanyabiashara kwa sababu wao ni wakusanyaji na walipaji wa kodi hiyo kwa niaba ya Serikali. Mzigo halisi wa VAT unabebwa na mtumiaji wa mwisho anayenunua bidhaa au huduma.
Kwa bidhaa zinazoingizwa nchini, mtu aliyelipa VAT wakati wa kuingiza bidhaa anaweza kudai VAT hiyo kama mkopo wa VAT ya manunuzi. Pia, VAT iliyolipwa chini ya sheria ya VAT ya Zanzibar kwa bidhaa zinazohamishiwa Tanzania Bara inaweza kudaiwa kama mkopo wa VAT ya manunuzi, endapo masharti yaliyowekwa na sheria yametimizwa.
Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
Marejesho ya VAT
Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ni fedha anazorejeshewa mfanyabiashara. Mlipakodi atastahili kurejeshewa Kodi ya Ongezeko la Thamani iwapo katika kipindi husika cha mahesabu, taarifa zake za kodi zinaonyesha kodi kwenye manunuzi ni kubwa kuliko kodi kwenye mauzo. Marejesho huandaliwa na kulipwa kwa mlipakodi kupitia Mfumo wa Malipo kati ya Benki na Benki (TISS) au kupitia akaunti yake ya benki.
Mtu anayestahili kurejeshewa VAT ni yule ambaye VAT aliyolipa inazidi anayopaswa kulipa. Maombi ya kurejeshewa hufanywa kwa kuambatanisha:
- Cheti cha uhalisia kutoka kwa mhasibu aliyeidhinishwa na NBAA na TRA
- Hesabu za kiasi kinachodaiwa
Nyaraka kama: Bill of Entry, Airway Bill, EFD receipts, nk.
TRA italipa ndani ya siku 90.
MAREJESHO YA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI KWA WANADIPLOMASIA NA MASHIRIKA YA KIMATAIFA
Maombi ya kurejeshewa kodi kwa wanadiplomasia na mashirika ya kimataifa yatatumwa kwa Kamishna Mkuu
Je, Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Yanaweza Kufidia Kodi ambayo Haijalipwa?
Ndiyo. Marejesho yoyote ya kodi yanaweza kufidia kodi nyingine, adhabu, na riba ambazo mlipa kodi anayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, lakini Kamishna Mkuu atamjulisha mlipakodi kwa maandishi.
Je, riba inalipwa kwa marejesho yaliyocheleweshwa?
Ndiyo. Marejesho yanapaswa kufanyika ndani ya siku 30 baada ya tarehe ya kuwasilisha taarifa ya kodi kwa kipindi cha mwisho cha hesabu katika nusu mwaka au kupokea taarifa za malimbikizo ya mwisho ya kodi husika kwa kipindi chochote husika cha hesabu kinachoangukia ndani ya nusu mwaka huo, chochote kilichokuja baadaye isipokuwa kama Kamishna anaamini kuwa kuna hatari ya mapato. Kwa wafanyabiashara wanaolipa mara kwa mara marejesho yatafanyika ndani ya siku 30 baada ya tarehe ya kutoa taarifa ya kodi kwa kipindi husika cha hesabu, au tarehe ya kupokea taarifa ya kodi, yoyote iliyo ya baadaye. Iwapo marejesho hayo hayatafanyika katika kipindi hiki, riba inalipwa kwa mlipakodi katika benki ya biashara, kiwango cha mkopo kikiamuliwa na Benki Kuu.
Masharti Gani ya kuzingatia ili Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani yaweze Kufanyika?
Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani hayawezi kufanyika isipokuwa kama mwombaji amewasilisha miongoni mwa mambo mengine nyaraka na/au viambatisho vifuatavyo:
1. Hati ya uhalali inayotolewa na mkaguzi wa hesabu ambaye amesajiliwa na Bodi ya Wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini na ambaye amesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kama mshauri wa ya kodi.
2. Orodha ya taarifa za masuala ya maombi ya marejesho ya VAT inapaswa kujazwa na kukamilishwa kwa usahihi na mwombaji.
3. Kwa suala la wafanyabiashara wanaolipa mara kwa mara, nyaraka zifuatazo ni muhimu kuwasilishwa:
- Hati ya tamko la uingizaji wa bidhaa (TANSAD)
- Hati ya taarifa ya mizigo iliyopo kwenye meli
- Hati ya kusafirishia mizigo kwa Ndege
- Hati ya taarifa ya mizigo inayosafirishwa kwa njia ya barabara
- Hati ya ardhi
Risiti/ankara za kielektroniki
4. Ripoti fupi ya mkaguzi wa hesabu kuonesha namna kiasi kinachodaiwa kimepatikana ikiwemo muhtasari wa manunuzi na mauzo.
Angalizo: Marejesho hayatakatwa/hayatatolewabaada ya miezi sita tangu tarehe ya Ankara ya kodi/risiti za EFD.
Nafuu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
Unafuu wa VAT kwa Mwekezaji chini ya EPZ, SEZ na Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi
Mwekezaji aliyepewa leseni chini ya uwanda wa mauzo ya nje au Sheria za eneo maalum la kiuchumi ana haki ya kupata unafuu maalum wa VAT. Makampuni ya uchimbaji madini, mafuta na gesi yana haki ya kupata unafuu wa VAT mradi tu Kampuni ina makubaliano ya lazima na Serikali ambayo yanatoa unafuu wa VAT. Ili kufurahia Wawekezaji na makampuni yenye haki ya uchimbaji madini wanalazimika kujaza fomu: ITX263.02. E. Fomu inaweza kupatikana kutoka ofisi yoyote ya TRA iliyo karibu nawe au unaweza kuipakua kupitia tovuti ya TRA.
Kuahirishwa kwa malipo ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa za mtaji unamaanisha kuahirishwa kwa malipo ya VAT katika bidhaa za mtaji. Kuahirishwa kwa bidhaa za mtaji zilizoagizwa kutoka nje sio moja kwa moja kama ilivyo kwa maombi ya mwombaji; maombi yatachunguzwa na kuidhinishwa na Kamishna. VAT iliyohairishwa kwenye bidhaa mtaji iliyoagizwa lazima iwe na VAT inayozidi TZS 10,000,000. Hairisho hilo ni miaka kumi. Bidhaa zinazoingizwa nchini ambazo VAT yake ni chini ya 10,000,000/- zitachukuliwa kama kawaida na zitafuata kanuni za kawaida za ukokotoaji wa kodi kwa sheria na taratibu za Forodha.
Wazalishaji au waunganishaji wa bidhaa za mtaji zinazozalishwa nchini watatakiwa kutimiza masharti yaliyowekwa ili kupata hairisho la VAT ikiwemo kuajiri angalau wafanyakazi wenye ujuzi 100, wahandisi Watanzania watano, na kuwa na miundombinu ya uzalishaji yenye mashine na vifaa vinavyohitajika.
Msamaha wa VAT kwa miradi inayofadhiliwa na serikali au wafadhili
Kamishna Mkuu anaweza, baada ya maombi ya mwombaji katika fomu iliyowekwa, kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye;
(a) uingizaji wa malighafi zitakazotumika pekee katika utengenezaji wa vyandarua vya muda mrefu na mtengenezaji wa ndani wenye mkataba wa utendaji kazi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(b) uagizaji kutoka nje wa taasisi ya serikali au usambazaji kwa chombo cha serikali wa bidhaa au huduma zitakazotumika tu kwa utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na-
(i) Serikali;
(ii) mkopo wa masharti nafuu, mkopo usio na masharti nafuu au ruzuku kupitia makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali nyingine, mfadhili au mkopeshaji wa mkopo wa masharti nafuu au mkopo usio na masharti nafuu; au
(iii) mkataba wa ruzuku ulioidhinishwa ipasavyo na Waziri kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana ya Serikali iliyoingiwa kati ya mamlaka ya serikali za mitaa na mfadhili: Isipokuwa kwamba, makubaliano hayo yanatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa au huduma hiyo;
(c) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa ajili ya maafa ya asili au maafa/majanga.
(d) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa taasisi iliyo na makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa madhumuni ya kuendesha au kutekeleza mradi wa kimkakati: Isipokuwa kwamba, makubaliano hayo yanatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa au huduma;
(e) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa shirika lisilo la kiserikali lenye makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya mradi unaotekelezwa na asasi isiyo ya kiserikali inayohusika: msamaha kwa bidhaa au huduma.
Kumbuka:
Msamaha uliotolewa chini ya sehemu hii utakoma kufanya kazi na ushuru wa ongezeko la thamani utalipwa na kulipwa kana kwamba msamaha haujatolewa ikiwa bidhaa au huduma zilizotajwa zinahamishwa, kuuzwa au kutupwa kwa njia yoyote kwa mwingine. mtu asiye na haki ya kufurahia marupurupu sawa na yaliyotolewa chini ya Sheria hii.
Msamaha kwa Uwekezaji Ulioidhinishwa na NISC
Waziri, baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri na kwa agizo lililochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, atatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa au huduma kwa ajili ya utekelezaji wa uwekezaji maalum wa kimkakati ulioidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Uendeshaji Uwekezaji chini ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania.
Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
Msamaha wa VAT
Kamishna Mkuu anaweza, baada ya maombi ya mwombaji katika fomu iliyowekwa, kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye-
(a) uingizaji wa malighafi zitakazotumika katika utengenezaji wa vyandarua vya muda mrefu pekee.
(b) kuingiza au kusambaza kwa taasisi ya Serikali ya bidhaa au huduma zitakazotumika tu kwa utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na- (i) Serikali. (ii) mkopo wa masharti nafuu, mkopo usio na masharti nafuu au ruzuku kupitia makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali nyingine, mfadhili au mkopeshaji wa mkopo wa masharti nafuu au mkopo usio wa masharti nafuu. (iii) makubaliano ya ruzuku yaliyoidhinishwa ipasavyo na Waziri kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana ya Serikali iliyoingiwa kati ya mamlaka ya serikali ya mitaa na mfadhili: Isipokuwa kwamba, makubaliano hayo yanatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa au huduma.
(c) Uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa ajili ya kukabiliana na athari za majanga ya asili au maafa.
(d) Uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa taasisi yenye makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza au kuendesha mradi mkakati, endapo makubaliano hayo yanaweka masharti ya msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa au huduma hizo.
(e) Uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa taasisi isiyo ya kiserikali (NGO) yenye makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa mradi unaotekelezwa na taasisi hiyo pekee, endapo makubaliano hayo yanaweka masharti ya msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa au huduma hizo. Pia, uuzaji wa nyumba yenye thamani isiyozidi Shilingi milioni 50 unaofanywa na kampuni ya uendelezaji wa majengo (real estate developer).
(f) Usambazaji wa madini ya thamani, vito na mawe mengine ya thamani katika mitambo ya kusafisha madini (refineries), vituo vya ununuzi wa madini au katika Nyumba za Madini na Vito zilizoanzishwa na Tume ya Madini kwa mujibu wa Sheria ya Madini.
(g) Usambazaji wa ndege, injini za ndege, vipuri vya ndege na huduma za matengenezo ya ndege kwa waendeshaji wa usafiri wa anga wa ndani; pamoja na injini za ndege na vipuri vya ndege (isipokuwa vipuri vya bidhaa nyingine) vinavyotolewa kwa wazalishaji au waunganishaji wa ndege nchini au waendeshaji wa usafiri wa anga wa ndani.
(h) Usambazaji wa vifaa vya magari vinavyotumika kubadilisha mfumo wa matumizi ya mafuta ya magari kwenda kwenye mfumo wa gesi asilia au umeme kwa watu wanaojihusisha na ubadilishaji huo wa mifumo ya magari.
(i) Uingizaji wa vifaa vya kutengenezea maumbo (moulds) vinavyotumiwa na wazalishaji wa dawa nchini kwa matumizi maalum ya kutengeneza bidhaa za dawa katika Tanzania Bara.
(j) Vifaa vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi na kutumika katika vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme.
(k) Mitambo ya ndege aina ya turbojet, turbo-propeller, mitambo mingine ya gesi (gas turbines), pamoja na matairi mapya ya ndege.
(l) Vifungashio vya bidhaa za maziwa vinavyozalishwa nchini na vile vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi.
(m) Mita janja za LPG (gesi ya kupikia) zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
(n) Mafuta ya kula yanayozalishwa nchini kwa kutumia mbegu zinazozalishwa nchini.
(o) Nguo na mavazi yanayozalishwa kwa kutumia pamba inayolimwa nchini.
(p) Uzi wa polyester unaotumika mahsusi kwa ajili ya kutengeneza nyavu za uvuvi zilizoainishwa katika msimbo husika wa forodha.
Bidhaa zinazouzwa kati ya Bara na Zanzibar
Pale ambapo kwa upande wa usambazaji wowote wa bidhaa unaotozwa kodi, kodi ya ongezeko la thamani imelipwa Tanzania Zanzibar kwa kiwango cha chini kuliko kiwango kinachotumika Tanzania Bara, tofauti ya kodi ya ongezeko la thamani itahesabiwa kuwa haijalipwa. na zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoka kwa mtu anayetozwa VAT baada ya kuhamishwa kwa bidhaa kwenda Tanzania Bara.
Iwapo kuhusiana na usambazaji wowote wa bidhaa unaotozwa VAT, usambazaji huo unafanywa moja kwa moja na mtu anayetozwa VAT Tanzania Bara kwa mpokeaji ambaye ni mtu anayetozwa VAT Tanzania Zanzibar, Mamlaka ya Mapato Tanzania itakusanya kodi ya ongezeko la thamani na kuituma kwa Bodi ya Mapato ya Zanzibar.
Pale ambapo kwa upande wa usambazaji wowote wa bidhaa unaotozwa kodi, ushuru umelipwa Tanzania Zanzibar kwa kiwango sawa na kiwango kinachotumika Tanzania Bara, kodi hiyo itahesabiwa kuwa zimelipwa kwenye usambazaji unaotozwa kodi na hakuna kodi itakayolipwa baada ya uhamisho wake kwenda Tanzania Bara.
Wakala wa Kodi ya Zuio kwenye VAT
Kwa mujibu wa Sheria ya VAT, Wakala wa Kodi ya Zuio kwenye VAT ni Wizara Ya fedha, Taasisi za Serikali kama Wakala wa Serikali, Mamlaka za Udhibiti, Taasisi za Umma na Bodi zinazojifadhili kwa mapato yao, Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGA) na Vyuo Vikuu vya Umma, au mtu aliyesajiliwa ambaye ameteuliwa na Kamishna Mkuu kwa notisi.
Wakala huyu anatakiwa kuzuia sehemu ya VAT kutoka kwenye malipo anayolipa kwa wasambazaji waliyosajiliwa kwa VAT na kuwasilisha kiasi hicho cha VAT moja kwa moja kwa TRA.
Viwango vya Makato ya VAT:
- Bidhaa: Wakala atazuia 3% ya bei na kuwasilisha kwa Kamishna Mkuu, hivyo muuzaji atapokea 15%.
- Huduma: Wakala atazuia 6%, muuzaji atapokea 12%.
Endapo bidhaa au huduma zimeuzwa kwa mtu ambaye hajasajiliwa kwa VAT lakini analipa kupitia benki au mfumo wa malipo wa kielektroniki uliothibitishwa, kiwango cha VAT kitakuwa 16%.
Kamishna Mkuu atatoa notisi kwa umma kuainisha makundi ya watu wanaohusika na taratibu za utekelezaji wa mfumo huu.
Cheti cha Makato ya VAT
Wakala wa kuzuilia kodi anayehitajika kuzuilia VAT, baada ya kufanya malipo kwa msambazaji wa bidhaa au huduma zinazotozwa kodi na kukata kiasi husika cha VAT kinachopaswa kuzuiliwa, anatakiwa kuwasilisha marejesho na kulipa VAT iliyozuiliwa kabla au ifikapo tarehe 10 ya mwezi unaofuata. Baada ya VAT kuzuiliwa na kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakala wa kuzuilia kodi atampatia msambazaji Cheti cha Kuzuiliwa kwa VAT (VAT Withholding Tax Certificate) kilichozalishwa kupitia Mfumo wa IDRAS. Cheti hicho hutumika kama uthibitisho kwamba sehemu ya VAT ya mauzo (Output VAT) iliyotokana na usambazaji wa bidhaa au huduma zinazotozwa kodi imezuiliwa na kuwasilishwa moja kwa moja kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taasisi ya Serikali inayosaidia ukusanyaji wa Kodi
Taasisi ya Serikali inayosaidia ni nini?
Ni taasisi ya Serikali ambapo Kamishna Mkuu anaruhusiwa kukusanya malipo kwa niaba yake kwa bidhaa au huduma zinazotozwa VAT. Hii ni kwa taasisi kama Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Umma zinazotoa bidhaa/huduma kwa umma.
Kamishna Mkuu atatoa Cheti cha Kulipwa VAT kwa Mbele (Advance VAT Paid Certificate) kuthibitisha kuwa VAT imelipwa mapema kwa niaba ya taasisi hiyo. Cheti hiki kitakuwa na:
- Jina, anuani, TIN, VAT Reg. Number ya taasisi
- Tarehe ya kutolewa na kipindi cha kodi
- Namba ya cheti
- Maelezo ya bidhaa/huduma
- Kiasi cha malipo na VAT iliyojumuishwa
- Kiasi cha VAT ya awali iliyolipwa
Mchakato wa Kufuta Usajili
Mtu aliyesajiliwa ambaye ataacha kabisa kuuza bidhaa zinazotozwa kodi ya ongezeko la thamani ataomba kufuta usajili kwa njia iliyoainishwa katika kanuni. Maombi ya kufutwa kwa usajili yatafanywa ndani ya siku kumi na nne baada ya tarehe ambayo mtu huyo aliacha kabisa kuuza bidhaa zinazotozwa kodi ya ongezeko la thamani. Endapo Kamishna Mkuu ameridhika kwamba mtu anayeomba kufutwa kwa usajili hatakiwi kusajiliwa kwa kodi ya ongezeko la thamani na mtu huyo amesajiliwa kwa angalau miezi kumi na mbili, Kamishna Mkuu, kwa notisi ya maandishi, atamfuta mtu huyo usajili au chini ya miezi kumi na mbili, Kamishna Mkuu anaweza, kwa notisi ya maandishi, kufuta usajili wa mtu huyo, pale ambapo ataridhika kwamba inafaa kufanya hivyo. Kughairiwa kwa usajili wa mtu kutaanza kutumika kuanzia tarehe iliyowekwa katika notisi ya kughairiwa.
Kwa upande wa Mfanyabiashara Aliyekusudiwa,
Mfanyabiashara Aliyekusudiwa ambaye hatatii masharti ya kusajiliwa kwa VAT atamjulisha Kamishna Mkuu ndani ya muda wa siku 90 baada ya kumalizika kwa muda kwa kutoa sababu za kushindwa kuzingatia masharti. Na baada ya kupokea taarifa ya kushindwa kutekeleza, Kamishna Mkuu atamkabidhi mfanyabiashara aliyekusudiwa uamuzi wa maandishi, akieleza sababu za kukubali au kukataa kuongezwa kwa muda kama ilivyoombwa. Na pale Kamishna Mkuu anapokataa kuongeza muda, mtu huyo atachukuliwa kuwa amefutiwa usajili kwa madhumuni ya Kodi ya Ongezeko la Thamani kuanzia tarehe ya kuongezwa kwa muda huo. Na ikiwa mtu ambaye atashindwa kumjulisha Kamishna Mkuu atachukuliwa kuwa amefutiwa usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani.
Habari & Matukio
CTI NA TRA WAKUTANA KUTAFUTA SULUHISHO LA BEI YA SARUJI
TRA ITAENDELEA KUSIKILIZA NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIPAKODI