Emblem TRA Logo

WCO ESA KUENDELEA KUWAJENGEA UWEZO WA KITAALUMA MAAFISA FORODHA - DROCB JOSEPHINE MANYASI

11 May, 2026

Mkurugenzi wa Shirika la Forodha Duniani Ofisi ya Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA ROCB) Bi. Josephine Manyasi, amesema moja ya majukumu makubwa ya taasisi hiyo ni kuwajengea uwezo maafisa forodha kutoka nchi 24 wanachama wa Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA).

Akizungumza wakati wa Mkutano wa Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA Regional Meeting) uliofanyika Jumatatu Mei 11, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip - Zanzibar, Bi. Manyasi amesema WCO ESA imeweka mikakati mbalimbali inayolenga kuziwezesha Idara za Forodha katika nchi wanachama kuendelea kutoa huduma bora kwa wadau wa forodha kwa kuwajengea uwezo maafisa forodha katika maeneo mbalimbali.

Amesema mikutano hiyo, imekuwa jukwaa muhimu la kuziunganisha nchi wanachama kupitia kubadilishana uzoefu na ujuzi katika maeneo mbalimbali ya forodha ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa katika utekelezaji wa shughuli za kiforodha.

Bi. Manyasi ameongeza kuwa, WCO ESA inalenga kuhakikisha nchi zote 24 wanachama zinaenda katika mwelekeo mmoja hasa katika taratibu na mifumo inayosimamia shughuli za forodha ili kuongeza ufanisi, uwazi na ushirikiano baina ya mamlaka za forodha.

Aidha, amesema mafunzo kwa maafisa wa forodha yataendelea kutolewa kwa lengo la kuongeza weledi, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha huduma za forodha zinaendana na mabadiliko ya teknolojia na biashara duniani.

Nchi zinazounda WCO ESA ni pamoja na Tanzania, Botswana, Burundi, Comoro, Djibouti, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Kenya, Lesotho, Madagascar na Malawi.

Nchi nyengine ni Angola, Mauritius,  Msumbiji, Namibia, Rwanda, Sychelles, Somalia, Afrika ya Kusini, Sudani ya Kusini, Uganda, Zambia na Zimbabwe.