Emblem TRA Logo

TRA YAJA NA FURSA KUSIMAMIA MCHAKATO WA MASHINDANO YA MAWAZO BUNIFU

30 April, 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua rasmi awamu ya pili ya mashindano ya kupokea mawazo bunifu kutoka kwa umma, ikiwa ni hatua ya kupanua wigo wa kodi na kuboresha huduma za kikodi nchini. Kupitia mpango huo, zaidi ya washindi 1,020 wanatarajiwa kunufaika na zawadi mbalimbali za fedha taslimu, huku mshindi wa jumla akitarajiwa kujinyakulia kitita cha Shilingi milioni 50.

Akizindua mashindano hayo jijini Dar es Salaam Aprili 29, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alisema mpango huo unalenga kuwapa Watanzania nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika mageuzi ya mfumo wa kodi kupitia mawazo bunifu yatakayoongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato na kuboresha mazingira ya biashara.

Alisema mawazo yatakayowasilishwa yatasaidia utekelezaji wa mapendekezo 284 ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, huku akibainisha kuwa mafanikio ya awamu ya kwanza iliyoshirikisha washiriki 5,681 na kuibua wabunifu 9 bora yameongeza hamasa ya kuboresha zaidi awamu hii ya pili.

Katika kuimarisha uwazi na imani kwa washiriki, TRA imeunda kamati huru ya tathmini isiyohusisha watumishi wake, pamoja na kuboresha muundo wa zawadi. Maeneo ya kipaumbele ni pamoja na upanuzi wa wigo wa kodi katika sekta isiyo rasmi, urahisishaji wa ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wadogo, maboresho ya huduma za kidijitali na matumizi ya teknolojia katika utatuzi wa migogoro ya kikodi.

Kwa Wabunifu wote ili ushiriki tuma wazo lako bunifu kupitia tovuti ya TRA kipengele  cha innovation Apply na uwe sehemu ya mabadiliko na ujiweke katika nafasi ya kushinda

Kwa upande wao, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Mcha Hassan Mcha, na Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango, Dkt. Ephraim Mdee, walisema maboresho yaliyofanyika yanalenga kuongeza ubora wa mawazo yatakayopatikana, huku wadau akiwemo Makamu wa Rais wa TCCIA, Bw. Boniface Ndengo, akiipongeza TRA kwa kuendelea kushirikisha wananchi na sekta binafsi katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.