Emblem TRA Logo

TRA MBIONI KUANZA KUPATA TAARIFA ZILIZOFICHWA NA MAKAMPUNI YA NJE ILI KUKWEPA KODI

24 January, 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ipo mbioni kuanza kupata taarifa za walipakodi kutoka mataifa mengine hatua ambayo itaiwezesha kuwabana wanaoficha taarifa zao nje ya nchi kwa lengo la kukwepa kodi.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja baina ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda na wakaguzi kutoka Global Forrum wakiongozwa Mshauri wa Sera za Kodi Bw. Puneet Gulati kuhusu uwazi na kubadilishana taarifa za kodi kilichofanyika kwenye ofisi za TRA jijini Dar es Salaam Januari 23.2026.

Katika kikao hicho Kamishna Mkuu Mwenda amesema kwa kujiunga na mfumo wa kubadilishana taarifa za kimataifa moja kwa moja bila vikwazo kutaisaidia TRA kuyabana makampuni makubwa yanayoficha taafa zake nje ya nchi kwa lengo la kukwepa kodi hali itakayookoa mapato yanayopotea kupitia kuficha taarifa.

Amesema pindi TRA itakapoanza kupata taarifa hizo zitasaidia kuongeza uwazi utakaowezesha kuzuia ukwepaji kodi kimataifa na kuongeza mapato.

“Tunachotaka tukidhi vigezo vya kupata taarifa moja kwa moja bila kuomba ili tutumie taarifa hizo kuhakikisha kila kampuni inalipa kodi inayostahili na kutufanya tutende haki katika mfumo wa usimamizi wa kodi ambapo tunataka kabla ya mwisho wa mwaka 2026 tuwe tumekidhi vigezo” amesema Mwenda.

Amesema wanataka kutengeneza mfumo wa kodi utakaowezesha kila mmoja kulipa kodi inayostahili kwa walipakodi wa ndani na wale wa nje ya nchi, hali ambayo italeta usawa na kuongeza makusanyo ya kodi sambamba na kuimarisha uchumi wa nchi.

Awali Kamishna wa walipakodi wakubwa Bw. Michael Muhoja amesema wanataka kila mmoja alipe kodi kule alikopatia hela kwa kufuatilia taarifa zake na TRA itakapoingia katika utaratibu huo itaweza kukusanya kodi Zaidi na kuleta usawa.

Kwa upande wake Mshauri wa Sera za Kodi kutoka Global Forrum Bw. Puneet Gulati amesema anatarajia Tanzania itaendelea kupiga hatua kwa kufuata miongozo na mapendekezo yaliyotolewa ili kukidhi vigezo vya kupata taarifa za kimataifa moja kwa moja.

Amesema wanatarajia TRA itapata taarifa nyingi ambazo zitaisaidia katika utendaji wake na kuahidi kutoa ushirikiano mpaka pale itakapofanikisha maana tayari Tanzania ni mwanachana wa Global Forum ambaye alijiunga mwaka 2025 na ni miongoni mwa nchi wanachama 160 zilizojiunga na Umoja huo.

Timu hiyo ya wakaguzi imekuwepo nchini kukutana na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na binafsi kutoka Tanzania Bara pamoja na Zanzibar ambazo ni wadau muhimu wa utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya ubadilishanaji wa taarifa za kodi.

 Baadhi ya wadau hao ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania, Wizara ya Fedha , Benki Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Kuzuia Fedha Haramu, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni, Wakala wa Usajili na Ufilisi, Wizara ya Fedha Zanzibar, Mamlaka ya Usajili wa Biashara Zanzibar, Mamalaka ya Mapato Zanzibar, Kamisheni ya Wakfu na Amana Zanzibar pamoja na Mwanasheria Mkuu Zanzibar, wawakilishi wa Mabenki, Wawakilishi wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu pamoja na Wawakilishi wa Wanasheria.