Emblem TRA Logo

TRA YAWAPATIA BAJAJI WATUMISHI WENYE ULEMAVU ILI KURAHISISHA HUDUMA KWA WALIPAKODI

12 September, 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa Bajaji kwa Watumishi wake wenye mahitaji maalum ili kuwarahisishia mazingira ya kufika kazini kwaajili ya kutoa huduma bora na wakati kwa walipakodi.

Bajaji hizo zimekabidhiwa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda Septemba 11, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifunga mafunzo kwa watumishi wenye mahitaji maalum na kueleza kuwa vitendeakazi hivyo vimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuboresha huduma kwa walipakodi maana vitawawezesha Watumishi hao kufika kazini kwa wakati na kwa usalama.

Amesema TRA imekuwa ikitoa huduma kwa usawa kwa watumishi wake wote bila kujali hali zao na kuwa itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa watumishi wenye mahitaji maalum ambao amewapongeza kwa kuwa familia ya TRA kutokana na uwezo wao na kusema Mamlaka inawategemea .

"TRA ina jumla ya watumishi 44 wenye mahitaji maalum na wakati naingia TRA kulikuwa na watumishi wenye ulemavu 18 hivyo idadi ya watumishi hao itaendelea kuongezeka" amesema Bw. Mwenda.

Miongoni mwa waliokabidhiwa Bajaji ni mtumishi wa TRA Bi. Hope Nsalu ambaye amesema awali alikuwa anatumia usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda lakini usafiri aliopatiwa utamsaidia kumfikisha kazini mapema na kwa usalama na kumshukuru Kamishna Mkuu kwa kuendelea kuwajali watumishi wenye mahitaji maalum.

"Namshukuru sana Kamishna Mkuu maana sasa hivi nitakuwa na uwezo wa kujitegemea katika shughuli zangu hali itakayoniongezea ufanisi zaidi katika kuwahudumia walipakodi na kufika kazini kwa wakati na kwa usalama " amesema mtumishi huyo.

Watumishi waliopatiwa Bajaji wameishukuru TRA kwa kuendelea kuwajali na kuahidi kuendelea kutoa  huduma bora kwa walipakodi.