Emblem TRA Logo

TRA MSHINDI WA JUMLA UANDAAJI WA MAHESABU TUZO ZA NBAA 2025

05 December, 2025

Mamlaka ya Mapato tanzania (TRA), imeibuka Mshindi wa kwanza wa jumla katika tuzo ya Uandaaji wa Hesabu za Kifedha zinazozingatia viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS), kwa mwaka 2024 zilizotolewa na  Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) tarehe 04.12.2025 Bunju jijini Dare es Salaam.

Pia TRA imeibuka mshindi wa kwanza katika tuzo ya  kipengele cha Taasisi za Serikali (Government Agency Categories) katika tuzo hizo.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo hizo, Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Luswetula,  alizipongeza taasisi zilizoibuka na ushindi, huku akisema wizara hiyo itaendelea kutoa ushirikiano kwa NBAA, ili kuendelea kuzalisha wahasibu na wakaguzi bora.

Sambamba na hayo Mhe. Luswetula amesema serikali itahakikisha NBAA inasimama imara ili iendelee kuzalisha watendaji bora kwa maslahi mapana ya taifa.

Naye Naibu Kamishina Mkuu  wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha amesema, tuzo walizozipata zina umuhimu mkubwa, kwani zinachangia kuonesha utendaji wa TRA namna unavyokubalika kimataifa.

Pia amesema tuzo hizo zinaonesha umahiri na ubunifu ulioopo kwa watumishi wa mamlaka hiyo.

"Tuzo hizi zina umuhimu sana kwetu, zinachangia kuonesha kuwa utendaji wetu unakubalika kimataifa na inawaonesha walipakodi kwamba kila shilingi inayokusanywa inafika katika mfuko Mkuu wa Serikali." amesema

Vilevile Naibu Kamishna Mkuu Mcha, amewashukuru walipakodi kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwasababu TRA imeendelea kuvuka malengo ya ukusanyaji mapato kwa mwaka wa fedha uliopita 2024/25 na kwa mwaka huu wa fedha 2025/26 mpaka kufikia mwezi Novemba 2025, TRA imeendelea kuvuka malengo kwa miezi yote.

"Tunawashukuru sana walipakodi kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa Mwaka wa fedha uliopita ambapo tumevuka malengo, na pia kwa mwaka huu wa fedha ambao tunakwenda nao tumevuka malengo ya miezi yote mpaka kufikia mwezi Novemba" ameongeza Bw. Mcha

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA  Profesa Slyivia Temu amesema,  jumla ya taasisi 86 za umma na binafsi zimeshiriki katika kujipima ubora wa kuwasilisha taarifa za fedha kwa mwaka 2024.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA Bw. Pius Maneno amesema, lengo la tuzo hizo ni kuhakikisha taarifa za hesabu zinazotolewa zinakuwa na uwazi na uwajibikaji.

Amefafanua kuwa, tuzo hizo ni taarifa za hesabu za kuanzia Januari 2024 hadi Desemba 2024, ambazo zimezalishwa kwa kufuata hesabu za Kimataifa na zilizopata hati safi.