TRA YAZINDUA OFISI ZINAZOTEMBEA ILI KUSOGEZA HUDUMA KARIBU NA WANANCHI
02 March, 2026
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amezindua magari maalum ya kutolea huduma za kodi maarufu kama 'ofisi zinazotembea' lengo likiwa ni kuboresha zaidi utoaji wa huduma za kodi kwa kuzisogeza karibu na wananchi.
Akizindua magari hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka huduma za kodi zisogezwe karibu na wananchi Februari 25.2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar amesema yatasaidia kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za kodi na kurahisisha ulipaji wa kodi nchini.
Amesema magari hayo Mawili yatakayotumika kama "ofisi zinazohama" ambayo yamezinduliwa sambamba na magari mengine 72 ya kutolea huduma za kodi yatakuwa chachu ya ulipaji kodi kwa hiari maana huduma zitawafuata wananchi walipo bila kuwalazimu kuzifuata mbali.
"Nawapongeza TRA kwa ubunifu huu wa kuwafuata wananchi ili kuwahudumia katika maeneo yao hali hii itaongeza kasi ya ulipaji kodi sambamba na makusanyo ya kodi kuelekea kuiwezesha Tanzania kujitegemea kwa kiasi kikubwa kiuchumi maana tunapaswa kuisaidia nchi kimapato" amesema Balozi Khamis.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Uledi Mussa Abasi amesema huo ni miongoni mwa mikakati ya Mamlaka hiyo ya kujiweka katibu zaidi na wananchi na kuboresha huduma za kodi.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema uzinduzi wa magari ya ofisi zinazohama na magari ya kutolea huduma za kodi ni miongoni mwa mikakati ya kuimarisha huduma kwa walipakodi.
Amesema ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwataka kuendelea kusogeza zaidi huduma za kodi karibu na wananchi.
Amesema kupitia magari hayo mawili ya ofisi zinazohama na magari 72 ya kutolea huduma za kodi wataweza kuwafuata walipakodi na kuwapatia huduma zote za kodi katika maeneo yao.
"Magari haya ni ofisi zilizokamilika ambazo zitatoa huduma zote zinazopatikana kwenye ofisi nyingine za TRA na kutoa wito kwa wananchi kuyatumia magari hayo kupata huduma za kodi.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliohudhuria uzinduzi wa magari ya ofisi zinazohama za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamesema zitarahisisha utoaji wa huduma kwa kuwapatia huduma kwenye maeneo yao badala ya kulazimika kufuata huduma za kodi kwenye ofisi za TRA.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya uzinduzi wa magari hayo Mawili ya ofisi zinazohama kwenye eneo la Mwenge na Tegeta jijini Dar es Salaam sambamba na magari mengine 72 ya kutolea huduma ambayo yamegharimu kiasi cha Sh. Bilioni 24, wananchi hao wameipongeza TRA kwa kuendelea kuwa karibu nao kwa kuwasongezea huduma.
Wamesema kupitia magari hayo wafanyabiashara ambao bado hawajapata namba za utambulisho wa mlipakodi watapatiwa na kuingia katika mfumo wa kulipa kodi hali ambayo itaongeza wigo wa kodi sambamba na mapato ya Serikali.
"Tunashukuru mmezindua ofisi hizi ambazo tunaamini sisi wafanyabiashara wa sokoni Tegeta Nyuki zitatufikia na kutuwezesha kupata huduma za kodi ikiwemo TIN"alisikika Omar Hemed Mfanyabiashara wa Tegeta
"Tunaomba huduma za hizi ofisi zinazohama za kwenye gari zitufikie sisi waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda njiapanda ya Mabwepande ili tupate TIN kwa urahisi sambamba na Leseni za udereva" amesema Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Mabwepande.
Nako Mwenge mmoja wa wafanyabiashara aliyejitqmbulisha kwa jina la Ali Hamidu amesema kuzinduliwa kwa huduma ya ofisi zinazohama kutakuwa suluhisho la kufuata mbali huduma za kodi.
Magari hayo Mawili yaliyozinduliwa ni sehemu ya magari 10 ya ofisi zinazohama yanayotarajiwa kununuliwa na TRA ili kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za kodi ambapo thamani ya magari yote yaliyokabidhiwa leo ni Sh. Bilioni 24.
Hafla ya uzinduzi wa magari hayo imehudhuriwa na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara ikiwemo JWT na JWK ambao kwa niaba ya wafanyabiashara wengine wameahidi kuendelea kushirikiana na TRA katika masuala yote yanayohusu kodi ili kuwezesha ulipaji wa kodi kwa hiari.
Habari Mpya
WAZIRI WA FEDHA AKABIDHI TUZO ZA MAWAZO YA UBUNIFU ZA TRA
BANDARI KAVU SASA KUFANYA KAZI SAA 24
CG MWENDA AZINDUA BODI YA TRA UNITED
TRA YAFUNGUA KITUO KIPYA CHA HUDUMA ZA KODI MASAKI DSM