Emblem TRA Logo

TRA YAZINDUA DAWATI LA UWEZESHAJI BIASHARA DAR ES SALAAM

06 November, 2025

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda amezindua Dawati maalum la uwezeshaji biashara ambalo litasaidia kuwatambua Wafanyabiashara ambao hawapo kwenye mfumo rasmi na kutatua changamoto za Wafanyabiashara ili waweze kukuwa kwenye biashara zao. 

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 27.09.2025 katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, Viongozi Wafanyabiashara na vikundi mbalimbali vya wajasiriamali. 

Bw. Mwenda amesema kuwa, kuna baadhi ya wafanyabiashara wanachagamoto za kikodi na hawajui pakuzitatua lakini dawati hilo litaweza kuwasikiliza na kuwatatulia changamoto zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Edward Mpogolo akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Edward Chalamila, alisema dawati hilo litakuwa nyenzo ya kukuza uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla. 

"Tunapongeza TRA kwa hatua hii muhimu ya kuwasogezea huduma wafanyabiashara...Dawati hili litawawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kuwa wa kati, na wa kati kuendelea kuwa wakubwa. Hii ni njia ya kuongeza ajira na kipato kwa wananchi," amesema.

Kwa Upande wao, wafanyabiashara wamesema wamelipokea dawati hilo kwa mikono miwili, wakieleza kuwa linakwenda kuwa suluhisho ya changamoto zao.