TRA YATOA POLE KWA WALIOPATA CHANGAMOTO WAKATI WA UCHAGUZI
12 November, 2025
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda ametoa pole kwa Walipakodi, Watumishi wa TRA na Watanzania wote kwa ujumla waliopata athari mbalimbali zilizotokana na changamoto wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Akiwa ziarani katika mikoa ya Kikodi Ilala na Kariakoo ambako amezungumza wa walipakodi pamoja na watumishi, Kamishna Mkuu Mwenda amesema, TRA imeguswa na kilichotokea na kuwa itaendelea kutoa huduma bora na kuwasikiliza walipakodi pamoja na kutatua changamoto zao.
Amesema licha ya kuwepo kwa athari zilizowapata watumishi wa TRA na baadhi ya mali kuharibiwa, watumishi wanapaswa kuongeza weledi, ufanisi na uwajibikaji katika kuwahudumia walipakodi katika maeneo yao ili kuendeleza dhana ya kuwajali walipakodi.
“Sisi TRA kipaumbele chetu ni Walipakodi na biashara zao, kuhakikisha wao wapo salama na biashara zao zinaendelea kukua, hivyo natoa pole kwa wote waliopata changamoto na ninaahidi kuwa tutaendelea kuwa karibu nao na kuwasikiliza pamoja na kuwasaidia pale inapowezekana kwa mujibu wa Sheria, amesema Kamishna Mkuu Mwenda.”
Kamishna Mkuu Mwenda amesema katika maeneo ambayo ofisi zimepata changamoto huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida na tayari walipakodi wa maeneo husika wameshatangaziwa.
Miongoni mwa walipakodi waliozungumza na Kamishna Mkuu Mwenda ni Bw. Salim Virani wa Kariakoo, jijini Dar es salaam, ambaye amesema kuwa wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na TRA.
Mwisho.
Habari Mpya
IDRAS ITAONGEZA WIGO WA KODI NA KUSIMAMIA USAWA – CG MWENDA
MKUTANO WA TATHMINI YA UTENDAJI WA NUSU MWAKA
TRA YAKUSANYA TRILIONI 4.13 MWEZI DESEMBA PEKEE
IDRAS KULETA MAPINDUZI YA KIUTENDAJI TRA