Emblem TRA Logo

JUKWAA LA MAADILI TRA KUONGEZA HAMASA YA ULIPAJI KODI KWA HIYARI - NAIBU KAMSHNA MKUU TRA

24 April, 2026


Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Mcha Hassan Mcha, amesema uzinduzi wa Jukwaa la Maadili kwa wadau wa taasisi hiyo unatarajiwa kuongeza utiifu wa ulipaji kodi kwa hiari, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuisaidia nchi kujitegemea.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Maadili katika Ukusanyaji wa Kodi pamoja na uzinduzi wa jukwaa hilo, alisema TRA imeweka mkazo katika kujenga mazingira ya uwazi, uadilifu na uwajibikaji ili kuimarisha imani ya walipakodi.

Ameeleza kuwa jukwaa hilo litakuwa kiungo muhimu kati ya TRA, walipakodi na wadau wengine, likilenga kukuza maadili ya kazi na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.
“Tunatambua kuwa maadili ni msingi wa ufanisi wa taasisi yoyote. Kupitia jukwaa hili, tunalenga kuimarisha uwajibikaji wa watumishi wetu na kujenga uhusiano mzuri na walipakodi,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa TRA itaendelea kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani, kupambana na vitendo vya rushwa, pamoja na kubuni na kuendeleza mifumo ya siri ya upokeaji taarifa ili kudhibiti ukiukwaji wa maadili.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna Mkuu huyo, hatua hizo zitasaidia kuzuia vitendo visivyo vya kimaadili, kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa kodi na hatimaye kuwahamasisha wafanyabiashara na wananchi kulipa kodi kwa hiari.

Kongamano hilo limefanyika Aprili 24, 2026 katika Ukumbi wa Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, likihusisha wadau mbalimbali wa kodi na  kujadili namna ya kuimarisha misingi ya maadili katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.