Emblem TRA Logo

TRA YAWAKARIBISHA WAFANYABIASHARA WAPYA KUPATA MSAMAHA WA KODI MWAKA MZIMA

07 August, 2026

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda ametoa wito kwa wafanyabiashara wapya kwenda kusajili namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN) ili kupata msamaha wa kodi kwa mwaka mzima kama ilivyoelekezwa na Serikali wakati wa kupitisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Akiwa ziarani katika mikoa ya Kikodi Temeke na Ilala kwenye Kituo cha Kodi cha Chang'ombe jijini Dar es Salaam Agosti 06, 2026 Kamishna Mkuu Mwenda amesema msamaha wa kodi uliotolewa na serikali kwa nchi nzima kwa Wafanyabiashara wapya umeanza kutolewa Julai Mosi 2026.

Amesema utaratibu huo utasaidia kukuza biashara, kuongeza idadi ya walipakodi na kuwezesha biashara nchini huku akiwataka Walipakodi kuendelea kukitumia kitengo cha kuwezesha biashara ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

"Dawati la kuwezesha biashara kwenye kila mkoa na vituo vyetu vya kodi zinaendelea kutoa huduma za kuwezesha biashara kwa kutatua changamoto, kutoa ushauri na kuwaunganisha walipakodi na vyombo vya fedha hivyo endeleeni kulitumia kikamilifu" amesema Bw. Mwenda.

Kwa upande wake msimamizi wa Dawati la Uwezeshaji biashara mkoa wa Temeke Bi. Irene Lodia amesema dawati hilo kwa upande wa Temeke limekuwa likihudumia walipakodi wote wakiwemo wadogo,  wa kati na wakubwa na kueleza kuwa limesaidia kutatua baadhi ya changamoto.