KAMISHNA MKUU ASHIRIKI VIKAO VYA KAMATI YA KUMSHAURI WAZIRI WA FEDHA KUHUSU SERA ZA KODI
06 June, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, ameshiriki vikao vya Kamati za Kumshauri Waziri wa Fedha (Think Tank Committees) kuhusu Sera za Kodi vilivyofanyika tarehe 5 Juni, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage, Ofisi za Hazina, jijini Dodoma, vikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar.
Katika vikao hivyo, Serikali ilieleza kuwa imepokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wadau wa Serikali na Sekta Binafsi kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi, ada na tozo mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Mapendekezo hayo yanalenga kuimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kamishna Mkuu wa TRA ameshiriki vikao hivyo kama sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na wadau katika kuboresha mfumo wa kodi, kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza uchumi kupitia mapato ya ndani na sekta binafsi.
Kamati hiyo ya Kumshauri Waziri wa Fedha (Think Tank Committees) inaundwa na wataalamu na wawakilishi kutoka sekta mbalimbali ikiwemo Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali, pamoja na wadau wa Sekta Binafsi, wakiwemo wawakilishi wa taasisi za biashara, wawekezaji na vyama vya wafanyabiashara nchini.
Habari Mpya