TRA YAPONGEZWA KWA UZINDUZI WA DAWATI MAALUM LA UWEZESHAJI BIASHARA DODOMA
12 September, 2025
Dodoma
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imepongezwa kwa kuanzisha na kuzindua Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara, hatua ambayo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuimarisha mazingira ya biashara na kukuza uwajibikaji wa ulipaji kodi nchini. Uzinduzi huo umefanyika tarehe 11 Septemba 2025 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary S. Senyamule, alikuwa mgeni rasmi na kuongoza wageni waalikwa na kutoa pongezi kwa TRA kwa uamuzi wake wa kuanzisha dawati hilo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara.
“Nipongeze sana kwa hatua hii muhimu ya kuzindua dawati maalumu la kuwasikiliza na kuwawezesha wafanyabiashara kwa Mkoa wa Dodoma. Dawati hili litakuwa kiunganishi bora kati ya TRA na wafanyabiashara, litakuwa chachu ya kusikiliza kero zao, kutoa huduma kwa haraka na kwa ufanisi, na hatimaye kuchochea ulipaji sahihi wa kodi,” alisema Mhe. Senyamule.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kuwa dawati hilo litasaidia kupunguza changamoto ambazo mara kwa mara zimekuwa zikitajwa na wafanyabiashara kuhusu ucheleweshaji wa huduma na ukosefu wa mifumo wezeshi ya mawasiliano na hivyo litakuwa mwarobaini wa changamoto hizo na kuondoa vikwazo vya wafanyabiashara wengi Zaidi kusajiliwa kuwa walipakodi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, naye alisisitiza kuwa dawati la uwezeshaji biashara litakuwa msaada mkubwa katika kuondoa urasimu na kuhakikisha kero za wafanyabiashara zinashughulikiwa kwa wakati na kuongeza tija katika kukusanya mapato ya serikali yanayoiwezesha kuhudumia wananchi wake.
“Hili ni dawati la faraja kwa wafanyabiashara wote. Ni jukwaa mahsusi ambalo litawaunganisha moja kwa moja na mamlaka ili kupata majibu ya changamoto zao kwa uharaka na weledi. Hakika, hii ni hatua ya kuongeza uaminifu kati ya TRA na wafanyabiashara,” alisema Mhe. Shekimweri.
Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alieleza dhamira ya mamlaka katika kuendeleza uhusiano mzuri na wafanyabiashara kwa kuzingatia falsafa ya 4R zilizoasisiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambazo ni: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya.
“Mamlaka ya Mapato itaendelea kuwa rafiki wa wafanyabiashara wote nchini. Tutaendelea kutoa elimu ya kodi, kuhimiza ulipaji wa hiari, na kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa uadilifu na uwajibikaji mkubwa. Dawati hili ni ushahidi wa dhamira hiyo,” alisema Bw. Mwenda.
Hafla ya uzinduzi huo iliambatana na kaulimbiu isemayo: “Tunawatambua, Tunawasikiliza na Kuwawezesha,” ikimaanisha dhamira ya Mamlaka kuhakikisha kila mfanyabiashara anapewa nafasi ya kusikilizwa, kuthaminiwa na kuungwa mkono ili kuboresha shughuli zake.
Kaulimbiu hii inabeba maudhui ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza uzalishaji, kukuza ajira na hatimaye kuongeza mapato ya Taifa.
Uzinduzi wa Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa mikakati ya TRA ya kuboresha utoaji huduma, kuimarisha uwazi na uaminifu, na kuhakikisha kuwa ulipaji wa kodi unakuwa wa hiari na wenye tija. Dawati hili litaendelea kupokea malalamiko, changamoto na maoni ya wafanyabiashara, na kuyafanyia kazi kwa haraka kwa kushirikiana na taasisi husika ili kuhakikisha Taifa linaendelea kunufaika na kodi kwa maendeleo ya wananchi wote.
Kwa pamoja, viongozi na wadau walioshiriki hafla hiyo walikubaliana kuwa Dawati la Uwezeshaji Biashara ni nyenzo muhimu ya kukuza mshikamano kati ya TRA na wafanyabiashara, na ni mfano wa ushirikiano wa dhati unaolenga kukuza uchumi wa Taifa kupitia ulipaji sahihi wa kodi.
Mwisho.
Habari Mpya