Emblem TRA Logo

TRA IMEKUSANYA TRILIONI 37.957 KWA MWAKA WA FEDHA 2025/2026

02 July, 2026

Wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake tukio ambalo limeambatana na utoaji wa Tuzo za Rais kwa Mlipakodi Bora, imerekodi takwimu mpya za makusanyo ya kodi ya Sh. Trilioni 37.957 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na utolewaji wa Tuzo za Rais kwa Mlipakodi Bora Julai Mosi 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema makusanyo ya kodi ya Sh. Trilioni 37.957 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ni ongezeko la asilimia 105.24 ya lengo la kukusanya Sh. Trilioni 36.066 sawa na ukuaji wa asilimia 17.6.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema mafanikio hayo yamefikiwa kutokana na miongozo ambayo imekuwa ikitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuitaka TRA kujenga ushirikiano na walipakodi, kuimarisha mifumo ya kodi, kukusanya kodi bila kutumia mabavu na kuongeza mapato bila kuongeza viwango vya kodi.

Amesema wakati TRA ikitimiza miaka 30 inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Walipakodi ambao wamekuwa karibu na TRA na kulipa kodi kwa hiari.