BODI YA WAKURUGENZI TRA YAFANYA TATHMINI YA UTENDAJI KWA MWAKA WA FEDHA 2024/25
14 August, 2025
Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Uledi Mussa, imefanya kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/25 na kupitia mikakati ya utendaji iliyowekwa kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Kikao hicho cha siku mbili kimefanyika tarehe 11 na 12 Agosti 2025, katika ukumbi wa Malaika Hotel, jijini Mwanza, kikiwahusisha wajumbe wa bodi na wakuu wa idara za TRA. Katika kikao hicho, Bodi ya Wakurugenzi imepitia utendaji kazi pamoja na changamoto zilizojitokeza kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/25.
Miongoni mwa mafanikio yaliyobainishwa ni ongezeko la ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, ambapo TRA ilifikia zaidi ya lengo lake la ukusanyaji wa mapato kwa robo hiyo ya nne kwa mwaka wa fedha 2024/25 ikijumuisha mwezi Aprili hadi Mwezi Juni 2025 ambapo TRA ilikusanya Shilingi trilioni 8.22, ikizidi lengo la Shilingi trilioni 7.84, sawa na ufanisi wa asilimia 104.8.
Bw. Uledi Mussa ameipongeza TRA kwa utendaji mzuri na uboreshaji wa mifumo ya kielektroniki, ikiwa ni pamoja na TANCIS (Tanzania Customs Integrated System), ambayo imesaidia kupunguza mwingiliano wa ana kwa ana baina ya wafanyakazi wa TRA na walipakodi, na hivyo kuongeza uwazi na ufanisi katika huduma za forodha.
“TRA iko katika nafasi ya kuongoza juhudi za kitaifa za kufanikisha maendeleo endelevu ya Tanzania. Mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka wa fedha uliopita yanapaswa kuwa kichocheo cha kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kufikia malengo ya mwaka huu wa fedha 2025/26”, amesema Bw. Mussa.
Katika kikao hicho, Bodi imepitia mikakati ya TRA kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikilenga kuongeza mapato ili kufikia lengo lililowekwa na serikali la kukusanya shilingi trilioni 36.2. Mikakati iliyowekwa ili kufikia malengo ni pamoja na; Upanuzi wa wigo wa kodi, uimarishaji wa mifumo ya kielektroniki, elimu ya kodi, na mapambano dhidi ya magendo.
Bodi ya Wakurungezi ya TRA imeweka utaratibu wa kukutana kila robo ya mwaka wa fedha ili kufanya tathmini ya utendaji wa taasisi hiyo na kupitia mikakati ya utendaji itakayowezesha kufikia na kuvuka lengo la makusanyo.
Mwisho.

Habari Mpya