Emblem TRA Logo

TRA NA CTI KUSHIRIKIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA KODI

28 February, 2025

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeahidi kushirikiana na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) katika kutatua changamoto za Kodi zinazowakabili wamiliki wa Viwanda nchini ili kurahisisha shughuli zao.

Hayo yamejiri leo tarehe 27.02.2025 katika mkutano wa wamiliki wa Viwanda Jijini Dar es Salaam ambapo Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amewahakikishia ushirikiano wamiliki wa Viwanda na kuahidi kushirikiana nao.

Akijibu hoja mbalimbali za wamiliki wa Viwanda nchini wakati wa mkutano huo, Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA ipo kwaajili ya kusaidia ustawi wa Viwanda nchini kwa kutatua changamoto zinazowakabili Wamiliki wa Viwanda ili viendelee kukua zaidi na kuchangia pato la Taifa.

Bw. Mwenda amesema TRA inathamini mchango mkubwa unaotolewa na Viwanda kwenye uchumi wa nchi ikiwemo suala la ulipaji wa Kodi mbalimbali ikiwemo Kodi ya Mapato, ushuru wa Forodha na Kodi inayotokana na ajira za viwandani.

"Shauku yangu ni kuona ushirikiano baina ya TRA na Wamiliki wa Viwanda ili tuweze kutatua changamoto za Kodi kwa majadiliano na kukomesha matumizi ya Stempu Bandia kwa pamoja maana zimekuwa zikiathiri ushindani wa kibiashara sokoni" amesema Bw. Mwenda. 

Kamishna Mkuu Mwenda ameridhia ombi la Wamiliki wa Viwanda kupitia Shirikisho lao CTI la kuwa na mikutano ya pamoja ya mara kwa mara kwa lengo la kushughulikia changamoto zinazowakabili.

Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu Mwenda ameahidi kuongezwa kwa idadi ya mashine za ukaguzi wa mizigo inayoingia nchini ili kurahisisha zoezi la ukaguzi wa mizigo hiyo .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CTI Bw. Paul Makanza amesema wamiliki wa Viwanda wapo tayari kutoa ushirikiano kwa TRA ikiwemo kuwafichua wakwepa Kodi ambao wamekuwa wakisababisha kutokuwepo kwa ushindani uliosawa sokoni jambo linalochangia kuua Viwanda nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa CTI Bw. Leodeger Tenga amemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA kwa kukubali kukutana na wenye Viwanda na kuwasikiliza na kuelekeza kuwa mkutano huo utafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina yao.

Amesema tangu Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani kumekuwa na mabadiliko makubwa ndani ya TRA ambayo yameboresha utendaji kazi wa Viwanda ikiwemo matumizi ya Mifumo yaliyorahisisha kazi za wenye Viwanda na kuokoa muda.

Amepongeza kuimarika kwa mfumo wa TANCIS ulioboreshwa unaofanya kazi za Forodha, Viwanja vya Ndege na Mipakani ambako ndiyo mizigo mingi ya wenye Viwanda inakopita.

Mwisho.