Emblem TRA Logo

KAMATI YA WATAALAMU WA KODI YATAKIWA KUBORESHA SERA NA MBINU MPYA ZA UKUSANYAJI KODI AFRIKA MASHARIKI

23 September, 2025

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda ameitaka kamati ya wataalamu wa kodi kutoka Mamlaka za Mapato za Afrika Mashariki kuja na mapendekezo ya kuimarisha mifumo ya sera za kodi, kuwekeza katika mageuzi ya kiteknolojia na kulinganisha mifumo yao na viwango vya kimataifa ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato. 

Ameyasema hayo tarehe 22.09.2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 100 wa Kamati ya Wataalamu wa Kodi wa Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki (EARATC). Bw. Mwenda alisema mamlaka za kodi lazima ziwe wazi, karibu na walipakodi na zenye kuzingatia maslahi ya mlipakodi ili kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari.

“Ni wakati sasa tuwe na mtazamo wa mbele kwa kuimarisha sera, kuwekeza katika mageuzi ya kiteknolojia na kuoanisha mifumo yetu na viwango vya kimataifa; Mamlaka zetu zinapaswa kuwa wazi, rahisi kufikiwa na kumjali mlipakodi,” amesema.

Aidha, ametaja changamoto kuu zinazozikabili mamlaka hizo kuwa ni magendo, hatua za kifedha zisizo sawa zinazopingana na juhudi za ujumuishaji wa kikanda, biashara ndogo ya ndani ya kanda, kupungua kwa utii wa hiari wa kodi, pamoja na ugumu wa kutoza kodi kwenye uchumi wa kidijitali.

Hata hivyo, Bw. Mwenda amesema mafanikio yameanza kuonekana, akibainisha kuwa TRA imevuka malengo ya makusanyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa kukusanya trilioni 30.75 ikilinganishwa na lengo la trilioni 30.01, sawa na asilimia 102.44 ya utekelezaji.

Vilevile, amewapongeza walipakodi wa Tanzania kwa utii na ushirikiano wao, na kuwataka wajumbe wa EARATC kuendelea kuibua mbinu bora za kurahisisha ukusanyaji wa kodi kwa misingi ya haki na uwazi.

Mkutano huo wa 100 wa EARATC ulioshirikisha wawakilishi kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Tanzania unakusudia kujadili mbinu za kupambana na magendo, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuondoa changamoto za kikodi mipakani, na kuchochea ubunifu wa kiuchumi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwisho.