Emblem TRA Logo

KONGAMANO LA KODI LAWAVUTIA WADAU

10 May, 2025

Walipakodi walioshiriki Kongamano la Kodi Jijini Dar es Salaam tarehe 08.05.2025 lililoandaliwa na Chuo Cha Kodi wameeleza kuvutiwa na Kongamano hilo kutokana kuwapa nafasi ya kueleza kwa mapana changamoto zinazowakabili pamoja na kuainisha namna ya kuongeza wigo wa Kodi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Walipakodi hao akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Sevelin Mushi amesema uwepo wa Kongamano hilo umeendelea kuongeza wigo wa Elimu ya Kodi na kuwapa fursa Walipakodi kutoa mawazo yao ya namna ya kuongeza wigo wa Kodi na kuboresha mazingira ya ulipaji Kodi.

"Kwa mfano kule kwenye maeneo yetu ya Kariakoo wapo Wafanyabiashara wengi wazuri lakini elimu yao ni darasa la Saba, hivyo wakipatiwa vizuri Elimu ya Kodi wataweza kuwa Walipakodi wazuri na mabalozi kwa wengine, nimshukuru Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda mara kadhaa ametufikia, nanyi Chuo Cha Kodi mje" amesema Sevelin Mushi.

Rais wa Chama Cha Mawakala Tanzania (TAFFA) Bw. Edward Urio amesema Kongamano la Kodi litaongeza wigo wa mabalozi wa Kodi kupitia Elimu ambayo imetolewa hali ambayo itaendelea kuongeza wigo wa Kodi.

Rais wa Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania (TPSF) Bi. Angelina Ngalula naye ametoa mchango wake kwa kushauri kuwepo kwa Kampeni maalum ya kuwasajili bure Wafanyabiashara wote nchini itakayohusisha TRA, OSHA, Brela na Halmashauri ambapo watapatiwa vibali vyote bure hali itakayosaidia kuwatambua na kuanza kufanya ufuatiliaji na badae kuwawezesha kulipa Kodi.

Ngalula pia ameshauri kuendelea kutolewa kwa elimu ya Kodi ili iwe ni utamaduni kwa Watanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo mtu akinunua kitu hana haja ya kuomba risiti muuzaji anatambua kuwa ni wajibu wake kutoa risiti.

Awali akifungua Kongamano hilo Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanislaus Nyongo amesema kupitia Kongamano hilo TRA inakwenda kuongeza uelewa wa Watu katika kulipa Kodi jambo ambalo litasaidia kuongeza wigo wa Kodi.

Mhe. Nyongo amesema Kongamano hilo limekuja wakati muafaka ambapo TRA ipo katika mkakati wa kuongeza wigo wa Kodi na kuhamasisha ulipaji Kodi wa hiari.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema wameandaa Kongamano hilo ili kupata maoni na kushauri wa masuala ya Kodi kutoka kwa Walipakodi ambayo yatasaidia kufanya maboresho ya sera za Kodi na kuendelea kuwa na mazingira mazuri ya ulipaji Kodi nchini.

Amesema michango ya wadau walioshiriki Kongamano hilo ambayo imetolewa itafanyiwa kazi kwa kuzingatia kuwa miongoni mwa majukumu ya TRA ni kuwezesha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji.

Bw. Mwenda amewashukuru Walipakodi wote walioshiriki Kongamano hilo na kuwaomba kuwa mabalozi wazuri wa TRA.