WAMILIKI WA MALORI WAIPONGEZA TRA KWA KUWEZESHA BIASHARA YA USAFIRISHAJI
07 August, 2026
Chama cha Wamiliki wa Malori Nchini Tanzania (TATOA) kupitia kwa Mwenyekiti wake Bw. Elius Lukumay kimeipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kuwezesha biashara ya usafirishaji kwa kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwa Wamiliki wa malori wenye malori machache ambao wamekuwa wakikodiwa na wenye malori mengi.
Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja baina ya Viongozi wa TATOA na Menejimenti ya TRA Chini ya Kamishna Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda kilichofanyika katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam Agosti 07, 2026 Mwenyekiti wa TATOA amesema uamuzi uliofanyika unakwenda kuongeza wigo wa biashara za usafirishaji ndani na nje ya nchi.
Amesema kwa muda mrefu Wamiliki wa Malori wenye malori machache wamekuwa na kilio cha kuomba msamaha wa Kodi ya ongezeko la thamani kama ilivyo kwa wenye malori mengi lakini sasa wamepatiwa habari njema ambayo itaongeza wigo wa kodi kutokana na sekta ya usafirishaji kuwa kiungo katika sekta mbalimbali nchini.
"Tunaomba Kamishna Mkuu utufikishie shukrani zetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua hii kubwa itakayoleta mapinduzi kwenye sekta ya usafirishaji na kuongeza ajira nchini" amesema Lukumay.
Deogratius Massawe ni Kiongozi wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) aliyehudhuria kikao hicho ambaye amepongeza hatua zilizocgukuliwa kuwezesha biashara hiyo ya usafirishaji ambayo imekuwa ikivuka mipaka ya Tanzania.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema hatua hiyo ya Serikali imekuja ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuwezesha biashara ya usafirishaji nchini ambayo ina uhusiano mkubwa na biashara nyingine ndani na nje ya nchi.
Amesema TRA ipo kwaajili ya kuwezesha biashara na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ustawi wa biashara nchini huku ikitatua changamoto za kikodi na zisizokuwa za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara nchini ili kuwawezesha kupata faida nyingi zaidi na kuchangia katika ulipaji kodi.
Ametoa wito kwa wafanyabiashara wote wenye changamoto kutosita kutembelea ofisi za TRA ili kupata suluhisho la changamoto zinazowakabili na kuendelea kufurahia kufanya biashara nchini.
Habari Mpya
CTI NA TRA WAKUTANA KUTAFUTA SULUHISHO LA BEI YA SARUJI
TRA ITAENDELEA KUSIKILIZA NA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIPAKODI