TANZANIA NA MALAWI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA KODI MIPAKANI
07 October, 2026
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiongozwa na Kamishna wake Mkuu Bw. Yusuph Juma Mwenda na Mamlaka ya Mapato nchini Malawi (MRA) ikiongozwa na Kamishna Mkuu Bw. Felix Kingstone Tambulasi zimekubaliana kuendelea kuboresha huduma za kodi mipakani ili kuimarisha ushirikiano baina ya Mamlaka hizo.
Makubaliano hayo yametokana na mazungumzo baina ya Makamishna hao yaliyofanyika Oktoba 07, 2026 kando ya Mkutano wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA) unaoendelea kufanyika jijini Arusha ukiangazia matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ukusanyaji wa kodi baina ya nchi wanachama.
Katika mazungumzo hayo Kamishna Mkuu Mwenda amesema Tanzania na Malawi zinaunganishwa na mipaka mitatu ya Kasumulu, Isongole na Mbambabay hivyo ushirikiano wa kodi baina ya nchi hizo utawezesha biashara kwenye maeneo hayo na kukuza uchumi sambamba na makusanyo ya Kodi.
Naye Kamishna Mkuu wa MRA Bw. Tambulasi amesema kuboreshwa kwa huduma za kodi mipakani kutasaidia kukuza biashara baina ya nchi hizo mbili na kuwa Malawi imekuwa ikitumia Bandari ya Dar es Salaam hivyo kurahisishwa kwa mazingira ya kodi baina ya nchi hizo mbili kutasaidia kuwezesha biashara.