Emblem TRA Logo

TANZANIA MWENYEJI WA MKUTANO WA SHIRIKA LA FORODHA DUNIANI KANDA YA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA

08 May, 2026

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mara ya kwanza inakuwa mwenyeji wa mkutano  wa shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA) utakaofanyika kuanzia Mei 07 mpaka Mei 15 mwaka huu Visiwani Zanzibar na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 100 kutoka nchi wanachama wa umojas huo.

Akizungumza leo Mei 07, 2026 wakati wa ufunguzi wa vikao vya utangulizi Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa Bw. Juma Bakari amesema mkutano huo unafanyika nchini Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo mbali na manufaa ya kiforodha pia utakuwa na manufaa ya Kiuchumi kwa Tanzania kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ya utalii.

Amesema kupitia mkutano huo nchi wanachama wapatao 24 wanaounda umoja wa ESA watawasilisha taarifa za utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika kikao kilichopita na kujadili utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la uongozi la 31 yaliyotolewa mwezi Mei 2025 nchini Afrika Kusini.

Bw. Bakari amesema mkutano huo utabainisha mbinu bunifu za Forodha na kupokea taarifa kutoka taasisi mbalimbali za Forodha ili kufanikisha utekelezaji wa mpango mkakati wa shirika hilo.

"Mikutano hii inafanyika katika kipindi muhimu ambacho Afrika ina fursa kubwa ya kukuza biashara kwa kufuatia kuongezeka kwa mifumo ya kikanda na biashara za ndani ya Afrika, Mamlaka za Forodha zinapaswa kuwa chachu ya mabadiliko hayo" amesema Bw. Bakari.

Kwa upande wake Kiongozi wa shule ya Ushuru nchini Kenya ambaye ni miongoni mwa watoa mada Dk. Emma Omwenga amesema sheria zinazoongoza Idara za Forodha kote duniani ni moja kinachotofautiana baina ya nchi moja na nyingine ni viwango vya kodi.

Amesema wanatoa mafunzo ili kuhakikisha mipaka inalidwa sambamba na afya za wananchi wa mataifa husika kwa kuhakikisha bidhaa zisizoruhusiwa kuingia nchini haziingii.

Mkutano wa WCO ESA unatanguliwa na mkutano wa wakufunzi wa vituo vya mafunzo ya Forodha vya Kanda na kufuatiwa na  mkutano wa 43 wa wataalam wa masuala ya Forodha na kuhutimishwa na Mkutano wa 32 wa Baraza la Uongozi.