Emblem TRA Logo

MAONI YA SEKTA BINAFSI NI MUHIMU KUBORESHA MFUMO WA KODI NCHINI - CG MWENDA

12 May, 2026

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema maoni ya sekta binafsi yana mchango mkubwa katika kuboresha mfumo wa kodi nchini na kusaidia kujenga mazingira bora ya biashara na uwekezaji. Amesema hayo wakati wa warsha iliyowakutanisha TRA, sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo iliyofanyika katika ukumbi wa Four Points by Sheraton Dar es Salaam Jijini Dar es Salaam.

Bw. Mwenda amesema TRA inaendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa walipakodi na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi pamoja na wadau wa maendeleo ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Ameeleza kuwa maoni na ushauri wa wadau hao ni muhimu katika kuboresha sera, sheria na taratibu za kodi nchini.

Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya TRA na sekta binafsi umesaidia kuongeza uelewa wa masuala ya kodi na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari, hatua inayochangia kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha uchumi wa taifa. Ameongeza kuwa TRA itaendelea kusikiliza na kuzingatia maoni ya wafanyabiashara ili kujenga mfumo wa kodi wenye uwazi na ufanisi.

Kwa upande wake, Rais wa Chemba ya Taifa ya Wafanyabiashara Tanzania, Bw. Vicent Minja, ameipongeza TRA kwa kutoa nafasi kwa sekta binafsi kushiriki katika majadiliano ya kodi na biashara, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
Aidha, mwakilishi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani amesema ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ni msingi muhimu katika kuimarisha mifumo ya kodi na kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi nchini.