Emblem TRA Logo

MKUTANO WA TATHMINI YA UTENDAJI WA NUSU MWAKA

06 January, 2026

  • WAZIRI WA FEDHA AMPONGEZA MHE. RAIS KWA UWEKEZAJI WA MIFUMO YA KUKUSANYA KODI 

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji wa mifumo ya ukusanyaji wa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akifungua kikao cha tathmini ya utendaji kazi wa TRA kwa kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2025/2026 yaani Julai-Desemba tarehe 05.01.2026 jijini Arusha, Waziri wa Fedha amesema uwekezaji wa mifumo uliofanywa na Rais Samia umeleta mapinduzi katika makusanyo ya kodi. 

"Nampongeza sana Mhe. Rais kwa uwekezaji alioufanya katika mifumo ya kodi na matunda yake yamepatikana, mapato makubwa mliyokusanya ni matunda ya uwekezaji katika mifumo ya kodi" amesema Balozi Omar.

Amesema mifumo ya TRA imeunganishwa na baadhi ya taasisi na kutaka wale ambao bado hawajaunganishwa kuunganisha mifumo hiyo ili kuwezesha taasisi za Serikali kusomana jambo ambalo litarahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi.

Waziri wa Fedha amesema matumizi ya mifumo katika ukusanyaji mapato yataongeza uwazi na kuondoa mianya ya rushwa na ukwepaji kodi maana taarifa za walipakodi zitasomana kwenye mifumo yote.

Amesema hata makusanyo makubwa yaliyoifanya TRA kuvuka malengo kwa miezi 18 mfululizo yametokana na matumizi ya mifumo ya ukusanyaji kodi.

Aidha amepongeza utulivu uliopo katika kukusanya kodi na kutoa wito kwa TRA kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi ili kuongeza wigo wa kodi.

Katika hatua nyingine Balozi Omar ameitaka TRA kushirikiana na TISEZA katika kuweka mazingira ya kuvutia wawekezaji ambao badae watachangia kodi.

Kwa upande wake Kamishina Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda  amesema hali ya ulipaji kodi kwa hiari inaendelea kuimarika nchini, jambo linaloonesha mafanikio ya juhudi za utoaji wa elimu ya kodi kwa wananchi.

Amesema hivi sasa walipakodi wengi wanaona kulipa kodi bila kushurutishwa ni jambo zuri ambalo limeleta mafanikio katika ukusanyaji mapato na kuimarisha uhusiano kati ya TRA na wafanyabiashara.

Amesema pamoja na majukumu ya msingi ya kukusanya kodi, TRA imekuwa ikiweka mkazo katika kurahisisha huduma, kusikiliza walipakodi na kuboresha mazingira ya biashara, hatua ambazo zimeongeza imani ya wananchi.

Kamishna Mkuu ameahidi kuwa TRA itaendelea kushirikiana na walipakodi na wadau wengine kwa uwazi na weledi, ili kuendeleza mafanikio yaliyopo na kuchochea uwajibikaji wa hiari kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Kikao hicho ambacho hufanyika mara mbili kwa mwaka, awamu hii kimewahusisha viongozi wa vyama vya wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda na sekta binafsi ambao wamepongeza mwenendo wa TRA katika utendaji kazi wake na kuahidi kuendelea  kushirikiana nao kuongeza wigo wa kodi.

"Tupo tayari kushirikiana na TRA kuongeza wigo wa kodi kwa kushirikisha sekta binafsi" Rais wa TCCIA Bw. Vicent Minja

"Tunakiri kwamba tuna ushirikiano mzuri na TRA na tunaipongeza sana kwa makusanyo makubwa kuelekea kuiwezesha Tanzania kujitegemea kiuchumi" Bw. Hussein Sufian Mwenyekiti Shirikisho la Viwanda (CTI).

Rais wa Sekta binafsi TPSF Bi. Angelina Ngalula ameweka wazi kuwa mara kadhaa amekuwa na malalamiko dhidi ya TRA lakini kwa sasa hana malalamiko yoyote na kila kitu kinakwenda vizuri. 

Ngalula ameipongeza TRA kwa ukusanyaji mkubwa wa kodi usikuwa na mabavu ambao umeleta utulivu katika ukusanyaji wa kodi na ufanyaji biashara nchini.