"TUENDELEE KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI" MWANDUMBYA
21 November, 2025
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandumbya ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini na uwekezaji na kuitaka iendelee kutekeleza wajibu huo wenye tija.
Ameyasema hayo tarehe 21.11.2025 kwa niaba ya Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) wakati wa mahafali ya 18 ya Chuo cha Kodi cha TRA yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Katika mahafali hayo Mwandumbya amesema TRA imekuwa ikifanya kazi kubwa katika kuendesha nchi kwa kuwa na mchango mkubwa wa mapato ya ndani ya nchi huku Chuo Cha Kodi kikitumika kuwapika watumishi wa Mamlaka hiyo na kuwafanya wawe bora zaidi.
Amesema TRA imechangia kwa kiasi kikubwa utulivu wa biashara uliopo nchini ambao pia unaletwa na amani na utulivu na kuongeza kuwa suala la amani siyo la kisiasa ni suala la uchumi na lina uhusiano wa moja kwa moja na maisha ya wananchi.
Aidha ameunga mkono kauli iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda kuhusu kuongeza mapato yatokanayo na kodi kwa kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi na kuongeza wigo wa kodi huku walipakodi wazuri wakiwekewa mazingira rafiki.
Katika hotuba yake Kamishna Mkuu Mwenda amerejea hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akilizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa anataka Tanzania ijitegemee kiuchumi kwa kiasi kikubwa na kwamba kujitegemea hakuhusiani na kuongeza viwango vya kodi bali kuziba mianya ya ukwepaji kodi ili kuongeza mapato kwa maendeleo ya Taifa.
"Ieleweke kwamba nchi kujitegemea kwa kiasi kikubwa kiuchumi hakuhusiani na ongezeko la viwango vya kodi, tunachokifanya ni kuongeza juhudi katika kuziba mianya ya kodi na kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya" amesema CG Mwenda.
Amesema anaamini kuwa wahitimu hao wa Chuo Cha Kodi watakuwa mabalozi wa kuongeza ulipaji kodi wa hiari ili kuleta ustawi wa biashara nchini ambao unategemea kwa kiasi kikubwa amani na utulivu.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Uledi Mussa Abbas amewataka wahitimu hao kuhamasisha jamii kuendelea kulipa kodi kwa hiari maana ulipaji wa kodi ni uzalendo.
Amesema anatamani Chuo Cha Kodi kiwe kitovu cha umahiri cha masuala ya Kodi na Forodha Afrika ya kati kutokana na ubora wa hali ya juu wa mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.
Katika mahafali hayo yaliyohusisha wahitimu 561 baadhi ya wahitimu waliofanya vizuri wametunukiwa vyeti na kupatiwa zawadi huku wahadhiri waliofanya tafiti mbalimbali nao wakitunukiwa vyeti na zawadi.
Habari Mpya
IDRAS ITAONGEZA WIGO WA KODI NA KUSIMAMIA USAWA – CG MWENDA
MKUTANO WA TATHMINI YA UTENDAJI WA NUSU MWAKA
TRA YAKUSANYA TRILIONI 4.13 MWEZI DESEMBA PEKEE
IDRAS KULETA MAPINDUZI YA KIUTENDAJI TRA