DC KYELA AIPONGEZA TRA KWA KUKUSANYA KODI KWA UTULIVU NA KUWEZESHA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO
22 May, 2026
Mkuu wa wilaya ya Kyela iliyopo mkoani Mbeya Mhe. Josephine Manase ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuendelea kukusanya kodi kwa utulivu na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi ya TRA ikiongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Uledi Abbas Mussa na menejimenti ya Mamlaka hiyo ikiongozwa na Bw. Yusuph Juma Mwenda Mei 22, 2026 amesema wilaya ya Kyela inajivunia utekelezaji wa miradi ya maendeleo uliotokana na kodi za wananchi.
Amesema utulivu katika ukusanyaji wa kodi na ushirikishwaji wa walipakodi katika masuala mbalimbali ya kodi na utoaji wa elimu umeongeza imani ya wananchi kwa TRA na kuwafanya walipe kodi kwa hiari.
"Wilayani kwetu wafanyabiashara wanalipa kodi bila usumbufu hali ambayo imetuwezesha kufanya vizuri katika ukusanyaji wa kodi na kuvuka malengo yaliyowekwa na Serikali" amesema Mhe. Josephine. Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Uledi amemshukuru na kumpongeza Mkuu huyo wa wilaya kwa juhudi anazofanya kwa kushirikiana na watumishi wa TRA wilayani humo katika kuwezesha ukusanyaji wa kodi.
Amesema Bodi ya Wakurugenzi kwa kushirikiana na Menejimenti ya TRA wamekuwa wakiweka mazingira rafiki na rahisi katika ukusanyaji wa kodi hali ambayo imewezesha kuongezeka kwa ulipaji wa kodi kwa hiari nchini.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo itaendelea kuwezesha biashara kupitia Dawati maalumu la uwezeshaji Biashara, kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao ambapo ametoa wito kwa watumishi na viongozi wote wa TRA kwa nchi nzima, kuendelea kutoa huduma bora kwa walipakodi.
Habari Mpya