Emblem TRA Logo

KODI NI MSINGI WA MAENDELEO YA NCHI- WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO ZANZIBAR

12 August, 2026

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utendaji wake mzuri katika ukusanyaji wa mapato ulioiwezesha  kuendelea kuvuka malengo yaliyowekwa na Serikali huku akisisitiza kuwa kodi ni msingi wa maendeleo ya nchi na chanzo muhimu cha kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza alipokutana na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, katika Ofisi yake Vuga, Zanzibar, Waziri wa Fedha amesema mafanikio ya TRA yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, shule na viwanja vya michezo huku akimpongeza Kamishna Mkuu kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Dkt. Akil amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuunganisha mifumo ya TEHAMA ya TRA na Taasisi nyengine za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili iweze kusomana na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Amesema kusomana kwa mifumo ni muhimu katika kurahisisha huduma za kikodi, kuwezesha biashara pamoja na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema TRA itaendelea kushirikiana kwa karibu na ZRA katika kuboresha huduma za kikodi na kuwezesha biashara, sambamba na kushirikiana katika kukabiliana na wale wenye dhamira ya kukwepa kodi.

Amesema ushirikiano huo utaimarisha ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha walipakodi wanapata huduma bora na zenye ufanisi.

Pamoja na hayo Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaendelea kutumia Chuo cha Kodi kutoa elimu kwa watumishi wa taasisi mbalimbali kama vile ZRA na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya kodi, huku akieleza kuwa ni muhimu kuendeelea kuanzisha One Stop Centre, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kujenga mazingira rafiki zaidi kwa wafanyabiashara na wananchi.

TRA inadelea kusogeza huduma karibu kwa walipakodi na Siku ya kesho Agosti 12, 2026 itaweka jiwe la Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya TRA Kizimkazi, mkoa wa Kusini Unguja.