Emblem TRA Logo

UONGOZI WA SOKO LA HISA LA DSM WAIPONGEZA TRA KWA UTENDAJI KAZI MZURI

18 April, 2026

Mtendaji Mkuu wa soko la Hisa la Dar es Salaam Bw. Peter Nalitolela akiambatana na ujumbe wake wamekutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda ambapo wameipongeza TRA kwa utendaji kazi mzuri unaoiwezesha kuvunja rekodi ya makusanyo ya kodi kwa kuvuka malengo wanayowekewa na Serikali.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Aprili 17, 2026 katika ofisi za TRA Jijini Dar es Salaam Bw. Nalitolela amesema kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kwa upande wa TRA kunaashiria kuongezeka kwa uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na ukaribu uliopo baina ya TRA na Walipakodi.

"Mara kadhaa tumeshuhudia Kamishna Mkuu wa TRA akienda mpaka mikoani kwa walipakodi kuwasikiliza na kuwapa elimu ya kodi, hii imesaidia sana kukuza imani ya TRA kwa walipakodi na kukiona ni chombo chao, hivyo tunawapongeza sana kwa utendaji" amesema Nalitolela.

Amebainisha kuwa soko la Hisa la Dar es Salaam limesajili jumla ya taasisi 28 zikiwemo 22 za Serikali na wateja wao hao wamekuwa ni walipakodi wa TRA huku akiahidi kuendelea kushirikiana na TRA kutoa elimu ya kodi kwa wateja wa soko hilo la Hisa.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema TRA inatambua na kuthamini mchango wa Soko la Hisa la Dar es Salaam katika kodi na kuwa wataendelea kushirikiana nao katika kutoa elimu ya kodi kwa wateja wao na kuongeza wigo wa kodi.

Aidha amesema ili kurahisisha utendaji kazi baina ya TRA na Soko la Hisa la Dar es Salaam mifumo baina ya Taasisi hizo mbili inapaswa kusomana ili kukuza uwazi na kurahisisha utendaji kazi.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaendelea kuwezesha biashara na uwekezaji nchini na kutatua changamoto zinazowakabili walipakodi kwa wakati huku elimu ya kodi nayo ikiendelea kutolewa.