Emblem TRA Logo

BALOZI WA DENMARK APONGEZA KUPUNGUA KWA MALALAMIKO YA KODI NCHINI

17 April, 2026

Balozi wa Denmark nchini Tanzania Mhe. Jesper Kammersgaard amepongeza kupungua kwa malalamiko ya kodi nchini hali ambayo imechangiwa na juhudi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa karibu na Walipakodi, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.

Ameyasema hayo Aprili 17, 2026 jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda kwenye ofisi za Mamlaka hiyo.

Katika mazungumzo hayo Balozi Kammersgaard amesema katika siku za karibuni nchini Tanzania pamekuwepo na utulivu katika masuala ya kodi ambapo malalamiko ya walipakodi wa ndani na nje ya nchi yamepungua kwa kiasi kikubwa hali inayoonyesha kuridhishwa na huduma wanazopatiwa na TRA.

Aidha Balozi huyo amesema Denmark itaendelea kushirikiana na Tanzania kupitia TRA kwenye masuala  mbalimbali ya kodi ikiwemo elimu, kuzuia ukwepaji kodi pamoja na matumizi ya mifumo huku maeneo mengine yakitarajiwa kuendelea kuainishwa.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema kumekuwepo na ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo mbili kwenye masuala mbalimbali yakiwemo ya kodi ambapo TRA imenufaika kwa watumishi wake kujengewa uwezo katika masuala mbalimbali ya kodi.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA inatambua na kuthamini mchango wa kodi kutoka Denmark kupitia biashara na uwekezaji ambapo asilimia kubwa ya makasha yanayotumika kuingiza mizigo nchini yanatoka katika nchi hiyo na kuwa TRA itaendelea kuwezesha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.

Amesema wanatarajia kubadilishana zaidi uzoefu na Danish Tax Agency katika maeneo mbalimbali ikiwemo masuala ya usimamizi wa kodi, uchumi wa kidijitali, kuboresha zaidi mifumo na kuendelea kuongeza udhibiti ili kuzuia udukuzi kwenye mifumo.

Aidha Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA imepiga hatua kubwa kwenye matumizi ya mifumo baada ya kuzindua mfumo wa Kodi za ndani IDRAS pamoja na mfumo wa usimamizi wa shughuli za Forodha TANCIS ambayo imerahisisha zaidi ulipaji wa kodi na kuwezesha biashara.

Amesema TRA imekuwa ikiheshimu ushirikiano wa kikodi na mataifa mengine ikiwemo Denmark na itaendeleza ushirikiano huo.