CG MWENDA ATEMBELEA KIWANDA CHA SUKARI KILOMBERO, AAHIDI KUWEZESHA WAKULIMA WA MIWA
20 October, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amefanya ziara katika kiwanda cha Sukari cha Kilombero mkoani Morogoro na kuwahakikishia wakulima wa miwa kuwa TRA itawasaidia kuendelea kufanya biashara na viwanda vya Miwa na kuchangia maendeleo ya nchi.
Akiwa kiwandani hapo Oktoba 19, 2026 Kamishna Mkuu Mwenda amesema ataunda timu ya wataalamu kwaajili ya kuangalia mwenendo na taarifa za wakulima wa miwa wanaouza kwenye viwanda vya sukari ili kuwasaidia kuendelea kuuza miwa yao na kufuata sheria za kodi.
Amesema timu hiyo ambayo itafanya kazi kwa muda wa siku 30 itapitia kanzi data za viwanda vya sukari na kutoa ushauri wa namna bora ya kuwezesha biashara ya miwa kwa wakulima kwa kuwawezesha kupata namba za utambulisho wa Mlipakodi kwa urahisi.
Amesema TRA imedhamiria kuwezesha biashara kwa nchi nzima huku akikipongeza kiwanda cha Sukari cha Kilombero kwa kuzingatia sheria za kodi.
Naye Mkurugenzi wa Fedha wa kiwanda hicho Bw. Fakihi Fadhili amemshukuru Kamishna Mkuu kwa kuwatembelea na kuendelea kuwarahisishia mazingira ya ufanyaji biashara.
Amesema wamekuwa wakitekeleza kazi zao kwa malengo ya kuitosheleza Tanzania kwa sukari ili kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Habari Mpya
CG MWENDA: HAKUNA BIASHARA ITAKAYOFUNGWA KWA SABABU YA KODI
TANZANIA NA MALAWI KUENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZA KODI MIPAKANI