CG MWENDA AKUTANA NA MKURUGENZI WA TWIGA CEMENT , ASISITIZA KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WALIKODI
11 June, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema TRA itaendelea kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zao za kikodi kwa wakati ili kuwezesha mazingira bora ya biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kamishna Mkuu Mwenda ameyasema hayo Jumatano Juni 10, 2026 jijini Dar es Salaam, alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa Twiga Cement (TPC PLC), Alfonso Velez, katika mazungumzo yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na walipakodi wakubwa pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya kikodi.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA inaamini kuwa ushirikiano wa karibu na walipakodi ni msingi muhimu wa kujenga mfumo wa kodi wenye uwazi, unaozingatia mahitaji ya walipakodi na unaochochea maendeleo ya uchumi wa nchi.
Katika kikao hicho, viongozi hao walibadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya TRA na walipakodi kwa lengo la kuhakikisha mfumo wa kodi unaendelea kuwa rafiki kwa walipakodi huku ukichangia maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Bw. Velez aliipongeza TRA kwa kuendelea kujenga mazingira mazuri ya mazungumzo na ushirikishwaji wa wadau wa kodi, akibainisha kuwa hatua hiyo inasaidia kuongeza uelewa wa masuala ya kikodi na kuimarisha uhusiano kati ya mamlaka ya kodi na sekta binafsi.
Mazungumzo kati ya TRA na TPC PLC yanakuja katika kipindi ambacho TRA inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, maadhimisho yanayobeba kaulimbiu "Miongo Mitatu ya TRA, Mlipakodi Shujaa, Tanzania Inayojitegemea".
Habari Mpya